Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wachunguzwa kodi ya bil 99/-

5cc9b99d7d40ebb0e0495451d3e04f0b Wafanyabiashara wachunguzwa kodi ya bil 99/-

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha inachunguza wafanyabiashara wakubwa wanaodaiwa kukwepa kodi ya serikali shilingi bilioni 98.6.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, James Ruge, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa ni lazima fedha hizo za serikali zilipwe au kurejeshwa haraka iwezekanavyo.

Ruge alisema jijini Arusha kuwa, fedha hizo zinafuatiliwa kwa ukaribu kwa wafanyabiashara hao ili kuiwezesha serikali kutekeleza malengo muhimu ya maendeleo zikiwemo huduma za afya, elimu, maji, barabara na huduma nyinginezo.

Alisema hayo ofisini kwake wakati anatoa taarifa ya miezi mitatu ya utendaji kazi wa taasisi hiyo.

Alisema kazi hiyo ya ufuatiliaji wa urejeshaji fedha haifanywi na Takukuru pekee, inafanywa kwa kushirikiana na taasisi na Wizara za serikali kama vile Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Wizara ya Kilimo .

Ruge alisema, katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu imepanga mkakati kuchunguza fedha za NSSF shilingi milioni 326 ambazo ni makato ya michango ya watumishi katika sekta binafsi ambayo waajiri walikuwa hawafikishi katika mfuko huo kwa mujibu wa sheria.

Alisema operesheni hiyo kuwasaka waajiri wenye nia ovu kwa serikali inaanza mara moja na waajiri wote waliokata fedha za watumishi na hawakuziwasilisha NSSF kwa wakati watashitakiwa.

Ruge alisema hatua lazima zichukuliwe na waajiri wametakiwa kutimiza wajibu kwa mujibu wa sheria na si wanavyotaka wao.

Wakati huohuo Takukuru Mkoa wa Arusha inachunguza shilingi milioni 933.8 zilizokopwa na vyama vya kuweka na kukopa vya Kituo cha Mikutano ya Kimataifa (AICC) Saccos na cha Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Jiji la Arusha (AUWSA) Saccos.

Vyama hivyo vilikopa fedha hizo katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na hawakurejesha kwa wakati kama sheria inavyoelekeza. Ruge alisema AICC Saccos ilikopa sh milioni 435.7 na haikuzilipa kwa wakati.

Ruge alisema, Saccos ya AUWSA ilikopa shilingi milioni 498 na haikuzirejesha kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano hivyo Takukuru imeanza uchunguzi. Alisema fedha hizo mfuko wa PSSSF lazima zirejeshwe haraka iwezekanavyo.

Ruge alisema fedha hizo ni michango ya wananchi hivyo ni wajibu wa SACCOS hizo kurejesha fedha hizo kwa mujibu wa sheria kabla ya operesheni rejesha fedha za umma haijaanza rasmi.

Alisema taasisi hiyo pia ipo katika hatua ya kurejesha shilingi milioni 414 zilizotokana na mkopo wa matrekta uliotolewa na Mfuko wa Pembejeo wa Wizara ya Kilimo kwa wakulima 10 wa halmashauri ya Meru, Arusha na Monduli kati ya mwaka 2013 hadi 2016 .

Alisema fedha hizo zilitolewa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kwa lengo la kuwasaidia wakulima kuondokana na umasikini wa kutumia jembe la mkono.

Aliwataka wakulima wote wa mkoa wa Arusha waliopata mkopo wa matrekta wapuuze upotoshaji unaoenezwa kwamba mkopo wa serikali kuwa hairejeshwi.

''Natumia fursa hii kuwaasa wakulima wote mkoani Arusha waliopata mkopo wa matrekta, kupuuza upotoshaji huo na kurejesha fedha zote wanazodaiwa ili kufanikisha nia ya serikali ya awamu ya tano ya kuwawezesha wakulima wengi zaidi kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija'' alisema Kamanda Ruge.

Alisema fedha hizo ni muhimu kurejeshwa ili zitumike kukopesha wakulima wengine kama lengo la serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ya kuwezesha wakulima wengi zaidi kujikomboa kiuchumi.

Kamanda Ruge alisema baadhi ya wakulima waliokopeshwa mkopo huo tangu mwaka 2018 hawakurejesha mkopo huo na imebainika kuwa ni kutokana na kuhamasishwa na walaghai kuwa mikopo ya serikali huwa hairejeshwi.

Ruge alisema katika kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba hadi Desemba mwaka jana Takukuru mkoani Arusha imefanikiwa kurejesha fedha na mali zenye thamani ya Sh 578,580,334.

Alisema kati ya fedha hizo Sh milioni 365,580,334 ni fedha taslimu.

Alisema fedha hizo ni kodi ya serikali, madeni ya vyama vya ushirika na mali binafsi za wananchi zilizokuwa kwenye hatari ya kuzipoteza kutokana na ubadhirifu, dhuluma na utapeli.

Chanzo: habarileo.co.tz