Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wa familia moja matatani kwa mali ya wizi

49056 Pic+wafanyabiashara

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyabiashara watatu wa familia moja wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka  manne likiwemo la kukutwa na mali ya wizi yenye thamani ya Sh162,269,422.

Washtakiwa hao ni Samo Magweiga, Magweiga Munanka na Agnes Bukori.

Mbali na washtakiwa hao wengine ambao hawajafikishwa mahakamani hapo ni Anas Cholo (38) na Abuu Buseko (25). Hati ya kuwakamata washtakiwa hao imetolewa mahakamani hapo ili waje kujibu mashtaka yanayowakabili.

Wakisomewa hati ya mashtaka na  Wakili wa Serikali Simon Wankyo, amedai leo, Machi 27, 2019 kuwa washtakiwa pamoja na wenzao wawili ambao hawajafikishwa mahakamani, katika tarehe tofauti walifanya njama ya kuiba bidhaa ambazo zilikuwa zikisafirishwa.

Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa katika shitaka   la pili ambalo ni wizi wa bidhaa zilizokuwa zinasafirishwa, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 31, 2018.

Inadaiwa siku hiyo, walikutwa na bidhaa za wizi ambazo ni ndoo zenye rangi za kupaka kwenye nyumba zenye ujazo tofauti zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza.

Inadaiwa washitakiwa hao walikutwa na ndoo za rangi aina mbalimbali na zenye ujazo tofauti, matairi ya magari, jozi za viatu na kandambili, mali ya Athuman Abdallah vyote vikiwa na thamani ya Sh 162,269,422.

Shitaka la tatu ambalo ni shtaka mbadala la kuiba mali inayodaiwa kuwa ya wizi inayomkabili Samo, inadaiwa Septemba 21, 2018 eneo la Kariakoo mtaa wa Nyamwezi  alikutwa na bidha zinazodhaniwa ni mali ya wizi.

Pia katika shitaka la nne ambalo ni mbadala wa mashtaka tangulizi, linamkabili Agnes aliyeshtakiwa kwa kukutwa na mali inayodaiwa kuwa ya wizi.

Anadaiwa kutenda kosa hilo, Septemba 22, 2018 eneo la Kariakoo baada ya kukutwa na bidhaa hizo.

Washitakiwa walikana mashitaka hayo na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Shaidi alitoa masharti ya dhamana kwa kila mshitakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua ya utambulisho ikiwemo kitambulisho cha taifa na mmoja kati wadhamini hao atasaini dhamana ya Sh 30milioni.

Washitakiwa waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti na kesi yao itatajwa Aprili 23, mwaka huu.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz