Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara,fundi mbaroni uzushi vifo kwa corona

411f40d838702b9bf7211f00861eb7f2 Wafanyabiashara,fundi mbaroni uzushi vifo kwa corona

Tue, 23 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JESHI la Polisi mkoani Pwani, limewakamata watu wanne kwa tuhuma za kutumia mitandao ya jamii kueneza uvumi kwa kutaja watu waliodaiwa kupoteza maisha kutokana na virusi vya corona.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Wankyo Nyigesa, alisema jana kuwa, watuhumiwa hao na wengine wanaotafutwa walitaja na kupendekeza majina ya viongozi wa serikali ambao walitamani wafariki dunia.

Kamanda Nyigesa aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kuwa watuhumiwa hao walitumia mitandao ya kijamii kuwatisha wananchi.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Frank Nyange (47) ambaye ni fundi ujenzi mkazi wa Kongowe, na mfanyabiashara mkazi wa Kongowe, Mosses Mgao (34).

Watuhumiwa wengine ni mfanyabiashara mkazi wa Maili Moja Tangini, Mohammed Lutambi (45), na mjasiriamali mkazi wa Mkuza, Bumija Senkondo (55).

Alisema watu hao walikuwa wakiwatisha watu kuwa Watanzania wengi watakufa kwa sababu serikali haichukui tahadhari kuwalinda wananchi.

"Tunatoa rai kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, wananchi waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya," alisema Kamanda Nyigesa.

Alisema wananchi wanapaswa kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ikiwa ni pamoja na kutokutoa taarifa za uvumi kuhusu vifo vya watu na atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ilitangaza kuwa kuanzia jana ingeanza kuwashughulikia wapotoshaji kwenye mitandao wakiwemo wanaorudia kutuma taarifa za uongo zilizotumwa na watu wengine.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Faustine Ndugulile, alisema Dar es Salaam kuwa, watakaoshughulikiwa ni matapeli kwenye mitandao, wanaotoa taarifa za uzushi, uchochezi, na uzandiki.

“…sisi tumeshakubaliana kuanzia Jumatatu (jana) tutaanza kuchezesha watu muziki. Kwa hiyo nitoe rai kwa Watanzania kama huna uhakika na kile unachokisema usiposti, usiritwiti, usilaiki, usifanye chochote na wala usikomenti”alisema Dk Ndugulile na kuongeza;

‘Tutatoa namba mahususi za watu kulalamika kuhusiana na utapeli unaoendelea katika mtandao hiyo; taarifa tutaitoa lakini tunataka vilevile tutoe taarifa kuwana tutaanzisha zoezi la uhakiki wa laini zote za simu upya ili tuweze kubaini wale wote wanaoendelea kufanya hizi shughuli za utapeli na kuchukua hatua”alisema Dk Ndugulile.

Wakati huohuo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa juzi alionya wanaotumia mitandao ya kijamii kutoa lugha za matusi, kuudhi na pia kusambaza habari za uongo na upotoshaji.

Alisema jijini Arusha kuwa kufanya hivyo ni kinyume na kanuni za maudhui mtandaoni za 2018 zinazozuia watumiaji wa mitandao kutumia kufanya vitendo hivyo.

Chanzo: habarileo.co.tz