Wafanyabiashara sita wa Kariakoo Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya ukwepaji kodi na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh bilioni 8.6.
Washitakiwa hao ni Ibrahim Magenge (32) mkazi wa Kijichi, Eliyasau Mohamed (29) Mkazi wa Buza, Elisha Numvile (29), mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ali, Juma Samatta (47) mkazi wa Kigogo na Siraji Mtungule (32) mkazi wa Makongo Juu na Ofisa Mauzo.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Medalakini amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ritha Tarimo kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya ukwepaji kodi, matumizi yasiyo sahihi ya mashine za kielektroniki (EFDs) na kusababisha hasara.
Amedai kati ya Januari na Juni 29, mwaka huu maeneo ya Kariakoo, Ilala Dar es Salaam kwa pamoja walitoa risiti ya uongo kwa kutumia mashine ya kielektroniki ya EFD iliyosajiliwa kwa jina la Bupe Millinga yenye namba ya mlipakodi TIN 135-563-382.
Amedai katika mashine hiyo ilikuwa na taarifa za mauzo ya Sh bilioni 17.8 hivyo walikwepa kodi ya ongezeko la thamani ya Sh bilioni 5.3.
Pia amedai katika mashitaka ya pili, washitakiwa hao kwa pamoja walikwepa kodi ya ongezeko la thamani ya Sh bilioni 3.3 kwa kutumia mashine hiyo.
Katika mashitaka ya tatu na la nne, Medalakini amedai katika tarehe hizo washitakiwa walitumia mashine ya EFDs kukwepa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh bilioni 8.6.
Amedai kuwa kati ya Januari na Juni 29, 2022 maeneo ya Kariakoo Dar es Salaam, washitakiwa walitumia mashine isiyo sahihi ya Milinga kuonesha ina mauzo ya zaidi ya Sh bilioni 17.8 kwa lengo la kumdanganya Kamishna wa Mkuu wa TRA na kukwepa kodi ya Sh bilioni 3.3.
Pia amedai washitakiwa kwa pamoja waliisababishia TRA hasara ya Sh 8,691,535,718.50.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo, waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Medalakini amedai washitakiwa wanapaswa kuomba dhamana Mahakama Kuu kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana kwani kiasi cha fedha kimezidi Sh milioni 300.
Hakimu Tarimo ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 21 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wote wamerudishwa rumande.