Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara 12 kizimbani mauzo bila risiti

769347e59cf5d03e07f7fa392772f333 Wafanyabiashara 12 kizimbani mauzo bila risiti

Tue, 19 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa kikodi Kahama, imewafikisha mahakamani wafanyabiashara 12 wakidaiwa kuuza bidhaa bila kutoa risiti za kielektroniki (EFDs).

Washitakiwa hao pia wanadaiwa kutoa risiti zikionesha malipo pungufu pamoja na kuzuia maofisa wa TRA kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kahama, David Msalilwa alisikiliza kesi ya mshitakiwa Joseph Wabani.

Mshitakiwa huyo alikiri kosa la kufanya biashara bila mashine ya EFDs mahali pa wazi. Hakimu Msalilwa alimhukumu kifungo cha mwezi mmoja jela au alipe faini Sh milioni 1.5.

Hakimu Mkazi Wilaya Kahama, Donacian Agustino alisikiliza kesi ya mshitakiwa ambaye ni mmiliki wa duka la bidhaa la jumla, Lucas Kishimbe.

Mshitakiwa huyo alikiri kosa la kutotoa risiti za EFDs na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini Sh milioni tatu. Alilipa faini hiyo. Mahakama ilieleza kwamba washitakiwa wengine kesi zao zingeendelea jana.

Meneja wa TRA mkoa wa kikodi Kahama, Warioba Kanire aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, wameanza kuchukua hatua za kisheria kwa wafanyabiashara wasiotumia mashine za EFDs.

Alisema wafanyabiashara 12 tayari wamefikishwa mahakamani wakidaiwa kutokuwa na mashine za EFDs na wengine walidaiwa kutoa risiti zenye malipo pungufu kuliko fedha walizolipa wateja.

Alitaja baadhi ya washitakiwa hao kuwa ni Magnam Resources, Submarine Hotel, Kitapela Investment, Chillers Night Club, Emmanuely Kidenya, Juma Daud Saguda, Cosmas Joachim Mushi, Ushirombo Phamas, Bernad Kalamu Lyaka, Rivermak Hotel, Steven Mathias Masunga na Adelina Sylivester Mallya.

Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo alihimiza wananchi wadai risiti ya kila bidhaa au huduma wanayonunua.

"Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi kwa bidhaa wanazouza ama kwa kuacha kwa makusudi kutoa stakabadhi au kutoa stakabadhi yenye kiasi pungufu.

Hilo ni kosa kisheria na mhusika akibainika atatozwa faini ya Sh milioni 3 hadi Sh milioni 4 na iwapo ataendelea kukaidi, atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi," alisema Kayombo mjini Singida na kuongeza:

“Vivyo hivyo kwa mnunuzi ambaye hadai stakabadhi au anashiriki kuandaliwa stakabadhi yenye kiasi pungufu anastahili kupigwa faini ya Sh 30,000 hadi Sh milioni 1.5 kwa kosa hilo kulingana na thamani ya bidhaa aliyonunua.”

Chanzo: www.habarileo.co.tz