Mahakama ya Wilaya Kinondoni imewahukumu kifungo cha maisha jela, dereva wa Basi la Shule ya Starlight Pre & Primary, Alaphat Mtango (23) na Kassim Yusuph Geo (36) utingo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kubaka kwa genge ‘gange rape’.
Wawili hao wanadaiwa walimbaka mwanafunzi wa shule huyo maeneo ya Mivumoni Madale, aliyekuwa na miaka 6 ambapo kwa sasa ana miaka 8.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu, Amos Rweikiza baada ya kujiridhisha pasina kuacha shaka juu ya ushahidi wa upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi nane.
“Mahakama hii imejiridhisha pasina kuacha shaka, hivyo inawahukumu kifungo cha maisha jela, kama hamjaridhika na hukumu haki ya kukata rufaa ipo wazi,”
Katika kesi hiyo namba 392 ya mwaka 2022, upande wa jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Chesensi Gavyole na Salma Jaffari.
Kwa upande wa washtakiwa walikuwa na mashahidi wanne wakiwemo wao wenyewe, huku wakiwa wamewakilishwa na Mawakili Barnaba Rugua na Revocatus Sedede.
Kwa mara ya kwanza wawili hao walifikishwa mahakamani Novemba 29,2022 wakikabiliwa na mashtaka ya kubaka kwa genge, ambapo inadaiwa walimbaka mwanafunzi wa miaka 6 aliyekuwa anapanda basi hilo la shule ‘School Bus’ la StarLight Pre & Primary.
Inadaiwa wawili hao walimbaka mwanafunzi huyo kwa nyakati tofauti tofauti katika mwezi wa 11 mwaka 2022 maeneo ya Mivumoni, Madale.