JESHI la Polisi mkoani Tabora kwa kushirikiana na watumishi wa Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira (TUWASA), wamekamata watuhumiwa 21 kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa vifaa mbalimbali vya miundombinu ya maji na vingine tofauti.
Aidha, polisi wakiwa kwenye doria maeneo ya Miemba Kata ya Malolo Manispaa na Mkoa wa Tabora, wamewakamata watu wawili wakiwa na bangi debe tatu ndani ya mfuko ikiwa kwenye baiskeli.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao akitoa taarifa za mafanikio ya jeshi hilo kwa vyombo vya habari jana, alisema kwamba katika oparesheni zinazoendelea katika Manispaa ya Tabora na Mkoa wa Tabora walifanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vya miundombinu ya idara ya maji.
Alisema katika oparesheni hiyo, askari walikamata vifaa mbalimbali vilivyoibwa ikiwamo stendi za mita ya maji, koki, nondo, bomba, vipande vya mabomba ya barabarani, mabati, mizani ndogo, vitanda vya chuma vya mwochwari.
Kuhusu waliokutwa na bangi, kamanda alisema tukio hilo ni la Aprili 16, mwaka huu saa 2:00 usiku katika maeneo hayo ya Kata ya Malolo Manispaa ya Tabora. Alisema watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda Abwao alisema oparesheni zote za kukamata wahalifu wanaojihusisha na wizi wa miundombinu ya idara ya maji ni endelevu. Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwapatia taarifa za wahalifu wanaojihusisha na wizi huo