Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wanne Chadema warudishwa mahabusu, kesi kuendelea kesho

85039 Msigwa+pic Wabunge wanne Chadema warudishwa mahabusu, kesi kuendelea kesho

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga kesho Jumatano Novemba 20, 2019 kutoa uamuzi dhidi ya wabunge wanne wa Chadema waliokiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani bila taarifa yoyote.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Novemba 19, 2019 na hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya washtakiwa hao kumaliza kujitetea kwa nini  wasifutiwe dhamana baada ya kukiuka masharti.

Ijumaa iliyopita Novemba 15, 2019 mahakama hiyo iliamuru wabunge hao, Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); John Heche (Tarime Vijijini); Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda) kukamatwa baada ya kukiuka masharti ya dhamana kwa kutofika mahakamani kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili.

Mbali na kutoa amri hiyo, mahakama hiyo pia ilitoa hati ya wito kwa wadhamini  wao kujieleza kwa nini  hawakuwapeleka washtakiwa  mahakamani.

Wabunge hao wamerudishwa mahabusu na kutakiwa kufikishwa mahakamani hapo kesho saa 4:30 asubuhi ili mahakama hiyo itoe uamuzi.

Siku hiyo wenzao watano ambao ni mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji; naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) na Esther Matiko (Tarime Mjini) walifika mahakamani hapo.

Amri ya kukamatwa ilitolewa na Hakimu Simba baada ya washtakiwa hao kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote wala wadhamini wao.

Leo aliyeanza kujitetea ni Mchungaji Msigwa aliyedai kuwa alichelewa mahakamani baada ya gari alilokuwa akisafiria akiwa pamoja na Heche kupata ajali eneo la Dar Freemarket.

Amesema walilazimika kutumia usafiri wa pikipiki hadi mahakamani lakini walikuta kesi yao imeahirishwa.

"Hakimu naomba usinifutie dhamana kwa sina rekodi mbaya ya kuidharau mahakama,” amedai Msigwa.

Mahakama hiyo pia imeelezwa kuwa Mbowe ambaye ni  mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo amelazwa katika hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam tangu Novemba 17, 2019.

Hayo yameelezwa na Greyson Selestine ambaye ni mdhamini wa mbunge huyo wa Hai wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuendelea na utetezi.

Hata hivyo, Selestine hakueleza ugonjwa unaomsumbua Mbowe.

"Mbowe amelazwa Aga Khan tangu juzi na yupo chumba namba 507, nyaraka za matibabu tutaziwasilisha baadaye kidogo kwa sababu daktari bado anamhudumia hajaandaa ripoti. Kuna mwenzangu nimemuacha hapo hospitali ili ahakikishe anakuja na nyaraka hizo,” amesema Selestine.

Baada ya kueleza hayo upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi umemtaka  mdhamini huyo awasilishe nyaraka  za matibabu dhidi ya Mbowe.

Nchimbi amedai kuwa licha ya Mbowe kutokuwepo mahakamani hapo washtakiwa wengine wapo mahakamani hapo huku akigusia wabunge wanne ambao mahakama iliagiza wakamatwe, kutaka waieleze mahakama kwa nini walishindwa kufika mahakamani bila taarifa na ndipo alipoanza Mchungaji Msigwa kujitetea.

Katika kesi hiyo wote kwa pamoja wanakabiliwa na  mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.

Chanzo: mwananchi.co.tz