Dar es Salaam. Novemba 15, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliamuru wabunge wanne wa Chadema kukamatwa kwa kukiuka masharti ya dhamana na kushindwa kufika mahakamani bila taarifa.
Wabunge hao ni, John Heche (Tarime Vijijini); Mchungaji Pater Msigwa (Iringa Mjini), Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda).
Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya wabunge hao kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote wala wadhamini wao.
Mbali na amri hiyo, pia Hakimu Simba alitoa hati ya wito kwa wadhamini akiwataka kufika mahakamani hapo kujieleza kwa nini hawakuwapeleka washtakiwa mahakamani kama masharti ya dhamana yanavyotaka.
Kabla ya kutoa amri hizo, Hakimu Simba alisema Novemba 15, 2019, kesi ilipangwa kuendelea kusikilizwa saa 3 asubuhi na washtakiwa wengine waliwahi lakini hadi saa 4:05 washtakiwa hao wanne hawakuwapo mahakamani na hakuna sababu za msingi zilizotolewa.
"Kesi ilipangwa kuendelea saa 3:00 asubuhi lakini mpaka sasa saa 4 asubuhi hawapo wala mahakama haina taarifa zao," alisema Hakimu Simba.
Kabla ya kutolewa hati hizo, wakili wa utetezi, Faraji Mangula aliyewawakilisha mawakili Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala na Hekima Mwasipo, aliiambia Mahakama kuwa ana taarifa za Bulaya.
Hata hivyo, Hakimu Simba alimueleza kuwa wanayepaswa kuzungumza ni wadhamini wa washtakiwa hao si wakili.
Wakati Hakimu Simba akitoa amri hizo, baadhi ya viongozi wa chama hicho walitoka nje ya mahakama ya wazi namba moja kwa ajili ya kuwapigia simu ili kujua walipo wabunge hao.
Saa 4: 15 asubuhi, wakati kesi ikiwa imeshaahirishwa, Mdee, Msigwa na Heche waliwasili katika viwanja vya mahakama ya Kisutu na kukutana na wenzao wakitoka mahakamani.
Walipanga kwenda kuonana na hakimu aliyeahirisha kesi hiyo, lakini mpango huo haukufanikiwa.
Pia walienda ofisi ya waendesha mashtaka lakini waliambiwa kuwa amri imeshatolewa, hivyo wanasubiri utekelezwaji wa amri hizo.
Wajisalimisha
Novemba 16, Mdee alijisalimisha kituo cha Polisi Oysterbay, wakati Msigwa na Heche wakijisalimisha Kisutu Novemba 18, 2019 na kukamatwa na askari na kisha kuunganishwa na Mdee.
Waliunganishwa na Mdee aliyeletwa mahakamani hapo asubuhi akitokea kituoni ingawa washtakiwa hao hawakupandishwa mahakamani badala yake, walirudishwa Polisi Oysterbay kwa kuwa kesi yao ya msingi ilikuwa imepangwa kuendelea siku inayofuata yaani Novemba 19.
Hata hivyo, siku hiyo ya Novemba 18 jioni Bulaya naye alijisalimisha kituoni hapo na kukamatwa.
Wajieleza kwa nini wasifutiwe dhamana
Novemba 19, 2019 wabunge hao walipelekwa mahakamani wakitokea Polisi Oysterbay.
Saa 3:35 asubuhi kesi hiyo namba 112/2018 iliitwa na washtakiwa kuingia mahakama ya wazi namba moja wakiwa chini ya ulinzi na kisha kuungana na wenzao ambao walikuwa ndani ya mahakama.
Kabla ya kesi ya msingi kuanza, mahakama hiyo ilitoa nafasi kwa kila mshtakiwa kujieleza kwa nini asifutiwe dhamana.
Wakitoa sababu kwa nini wasifutiwe dhamana, Heche, Msigwa na Mdee waliieleza mahakama kuwa siku ya kesi walifika mahakamani kwa kuchelewa kutokana na sababu mbalimbali.
Msigwa na Heche walidai kupata ajali wakiwa njiani kwenda mahakamani hapo huku Mdee akidai aliugua ghafla akiwa njiani na kumlazimu kupitia hospitali na hivyo kuchelewa kufika.
Bulaya alidai hakufika mahakamani siku hiyo kwa kuwa alifiwa na mama yake mdogo hivyo alikwenda Singida kwa ajili ya mazishi.
"Wakati kesi inaendelea siku ya mwisho nilijaribu kunyoosha mkono lakini haukuniona hakimu, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Bunge baada ya kesi, nilikimbia kwenda Dodoma Alhamisi kwenye kikao ambacho kiliisha saa 1:30 nusu usiku na niliondoka saa 2:30nusu usiku na kuingia Dar es Salaam saa 2:30 asubuhi,” alisema Mchungaji Msigwa.
"Kwenye akili yangu nilijua kesi ni saa nne na nusu hivyo sikuwa na wasiwasi kama nitachelewa lakini nikiwa njiani kuja mahakamani nikiwa na Heche tulipata ajali eneo la Dar Freemarket.”
Mbunge huyo wa Iringa Mjini alisema, “hakimu ninaheshimu mahakama na siwezi kuidharau mahakama wala wewe binafsi, naomba mahakama isinifutie dhamana yangu.”
Kuhusu wadhamini wake kwa nini walishindwa kufika mahakamani hapo, Mchungaji Msigwa alidai kuwa mmoja wa wadhamini wake alijiondoa katika chama hicho.
Msigwa alidai mdhamini mwingine yupo Morogoro anauguza mama yake mzazi.
Mdee ameiomba mahakama isimfutie dhamana kwani anaiheshimu ila siku hiyo wakati anakuja mahakamani aliugua ghafla akapitia hospitali lakini kwa kuhofia kuchelewa alimpigia simu mdhamini wake ambaye naye alifika kwa kuchelewa.
Mdhamini wa Mdee, Matha Mtiko alidai kuwa wakati kesi inaitwa mahakamani, alienda chooni na wakati anatoka alikutana na washtakiwa wakitoka mahakamani kesi ikiwa imeahirishwa.
Naye Heche aliiomba mahakama hiyo isimfutie dhamana kwa sababu haikuwa dhamira yake kuchelewa.
"Mimi ninakaa Tarime karibu kilometa 1,600 kutoka Dar, hapa mjini sina familia wala mke, ila tangu kesi hii ianze sijawahi kuchelewa mahakamani wala kuonywa, ila siku ya kesi tukiwa njiani na Msigwa gari iligongwa, ikabidi tutafute sehemu ya kuiweka na kisha tukachukua bodaboda lakini tulipofika mahakamani tukakutana na wenzetu ndio wanatoka," amesema Heche.
Akifafanua zaidi, Bulaya alisema hawezi kuidharau mahakama, ila alipata msiba wa mama yake mdogo wilayani Mkalama mkoani Singida, hivyo aliwataarifu wadhamini wake ili siku ya kesi wafike, lakini nao walichelewa na kukuta kesi imeahirishwa.
Mdhamini wa Bulaya, Ndeshikulwa Tungaraza alidai wakati kesi hiyo anaitwa mahakamani, yeye alienda choo na wakati anatoka alikutaka na washtakiwa wanatoka mahakamani na kesi imeahirishwa.
Baada ya kumaliza kujitetea, upande wa mashtaka kupitia wakili wa Serikali, Salimu Msemo aliwasilisha hoja ya kutaka washtakiwa wafutiwe dhamana.
Msemo alidai ni muhimu suala la muda wa kuwepo mahakamani kuzingatiwa na ni dhahiri kuwa washtakiwa hawakuwepo mahakamani wakati kesi hiyo inaahirishwa.
"Hivyo ninaiomba mahakama iwafutie dhamana washtakiwa hao wanne na iwachukulie hatua stahiki wadhamini wao" alidai Msemo.
Akijibu hoja za upande wa mashtaka , wakili Kibatala alidai hakuna sababu za kimazingira wala kisheria za kufuta dhamana, uamuzi wa kutoa dhamana ni mwepesi zaidi kuliko uamuzi wa kuifuta.
Kibatala alidai kuwa hakuna ubishi kwamba wakati wa kesi hiyo washtakiwa walikuwa na rekodi nzuri ya kuhudhuria mahakamani na kwamba walitoa maelezo na siku ya kesi walikuja mahakamani.
“Ni kweli kwa kawaida kesi za jinai zinaanza saa tatu asubuhi lakini tangu waanze shauri hilo hawajawahi kuanza muda huo bali wamekuwa wakianza saa 4:30 asubuhi na kuendelea, kuchelewa mahakamani si kutofika,” amesema Kibatala.
Amedai kuwa mahakama si mashine kwa kuwa zipo sababu za kibinadamu na ndio maana kuna mahakimu au majaji wanaofanya maamuzi na kutafsiri sheria.
Akitoa uamuzi, Hakimu Simba alitoa onyo kali kwa wabunge hao akiwataka wasirudie tena kukiuka masharti ya dhamana.
Hakimu Simba alisema maelezo yaliyotolewa na washtakiwa hao na wadhamini wao hayajitoshelezi ila pamoja na hayo alijiongoza kusema kuwa kufuta dhamana za washtakiwa hao ni hatua kali sana.
"Maelezo yenu mliyoyatoa mahakamani hapa hayaingii akilini kitendo cha washtakiwa kujisalimisha polisi kilikuwa ni kuogopa nini kitatokea," amesema Hakimu Simba.
Mbali na onyo hilo, aliwataka Msigwa na Heche tarehe ijayo wawapeleke wadhamini wao mahakamani.
Kesi hiyo itaendelea kuanzia Novemba 26 hadi 29, 2019 na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Washtakiwa hao pamoja na viongozi wengine wa chama hicho akiwamo mwenyekiti, Freeman Mbowe wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.