Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge CCM mbaroni kwa tuhuma za rushwa

73744 Takukuru+pi Wabunge CCM mbaroni kwa tuhuma za rushwa

Fri, 10 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WABUNGE wawili kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliomaliza muda wao, wamekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma kwa tuhuma za kutoa hongo kwa watu wanaosadikiwa kuwa wajumbe wa chama hicho.

Akizungumza na Nipashe jijini hapa jana, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, aliwataja wawili hao kuwa ni aliyekuwa Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba.

Kibwengo, akifafanua kuhusu tuhuma dhidi ya Lusinde, alisema TAKUKURU ilipata taarifa Julai 7 mwaka huu kwamba alikuwa amewakusanya wajumbe wa CCM nyumbani kwake Mvumi wilayani Chamwino mkoani hapa, kwa ajili ya kuwahonga na kufanya ushawishi fulani.

Alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, maofisa wa taasisi hiyo walifika katika nyumba hiyo na kukuta watu wanaosadikiwa kuwa ni wajumbe wa CCM takribani 20.

"Wajumbe hao walikutwa nyumbani kwa mtuhumiwa, hatukukuta wakigawana fedha kama taarifa zilivyoeleza, isipokuwa walikuwa wameandaliwa chakula na walipoulizwa, walisema walikwenda huko kumwona mtu ambaye amejifungua.

"Lakini, kama tunavyojua, ukienda kumsalimia aliyejifungua, huwezi kwenda bila zawadi, hao wote hawakwenda na chochote,” alisema.

Alisema kuwa baada ya kutilia shaka maelezo yao, maofisa hao walimkamata Lusinde na kuwekwa chini ya ulinzi na kusitisha mkutano wake na wajumbe hao.

“Suala lake lina picha mbili; kwanza wamsaidie yeye mtia nia na jingine wamsaidie Halima Okash ambaye ni mtia nia ya kugombea ubunge wa viti maalum. Kwa hiyo, yote tunaendelea na uchunguzi kuthibitisha hizi taarifa, lakini kwa sasa Lusinde ameachiwa.

"Lusinde alihojiwa jana (juzi), lakini atahojiwa tena leo (jana) au kesho (leo) kadri uchunguzi unavyoendelea. Pia, tunaye huyo Halima Okash, tunaendelea naye kwa mahojiano," alisema.

Kuhusu tuhuma dhidi ya Serukamba, kiongozi huyo wa TAKUKURU alisema wanamshikilia kwa tuhuma zinazofanana na za Lusinde, ikidaiwa kuwa naye alikuwa akigawa rushwa zinazohusiana na Uchaguzi Mkuu kwenye Hoteli ya Dodoma.

Kibwengo alisema wanaendelea na msako wa watia nia wote wanaotegemea rushwa kushawishi kupitishwa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live