Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vita dhidi ukeketaji watoto wa kike yaonesha mafanikio

Cf5775173fca069d0483c0ee485c1db2 Vita dhidi ukeketaji watoto wa kike yaonesha mafanikio

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

VITA dhidi ya ukeketaji watoto wa kike, imeanza kuonesha mafanikio mkoani Singida, baada ya wazazi wa kike waliokuwa wakituhumiwa kuwa kikwazo katika suala hilo, kuanza kujitokeza hadharani kupinga mila hiyo potofu na yenye madhara makubwa kiafya.

Awali ilielezwa kuwa licha ya juhudi kubwa za serikali na mashirika kupambana na mila hiyo potofu, wazazi wa kike waliendelea kuwa kikwazo kwa kubuni mbinu mpya ya ukeketaji watoto wachanga kwa siri ili kukwepa mkono wa sheria.

Ilielezwa kuwa baada ya serikali kutunga sheria inayotaja ukeketaji kuwa kosa la jinai, baadhi yao walianza kufanya kitendo hicho kwa siri usiku wa manane kwa kumsugua mtoto mchanga sehemu zake za siri kwa majivu au chumvi aina ya magadi hadi damu itoke au kukata kwa kucha sehemu hiyo ili kutekeleza mila hiyo potofu.

Hata hivyo, Mratibu wa Shirika la ESTL linalotekeleza mradi wa kupinga ukatili wa kijinsia wilayani Singida, Filbert Swai alisema kuwa baada ya elimu kutolewa zaidi, sasa yapo mafanikio yaliyoanza kujitokeza kutokana na baadhi ya ngariba, wazazi na walezi wa kike, kuanza kupinga mila hiyo hadharani.

“Iwapo wazazi wa kike na baadhi ya ngariba ambao ndio walikuwa vinara wa kufanya jambo hilo kwa siri usiku wa manane, sasa wameanza kutoka mchana kweupe na kutangaza kupinga mila hiyo kwenye mikutano ya hadhara ni dhahiri kuwa vita hii tunaenda kushinda,” alisema.

Ngariba mstaafu, Halima Ntandu (76) mkazi wa Ntuntu wilayani Ikungi alisema kuwa yeye ameacha kufanya ukeketaji baada ya kupata elimu kupitia vyombo vya habari na mikutano ya hadhara juu ya madhara ya ukeketaji na hatua zinazoweza kuchukuliwa iwapo mtu atabainika anakeketa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani alisema kuwa ingawa vitendo hivyo vimeanza kupungua, mila hiyo bado ni kikwazo cha ulinzi na usalama wa mtoto mkoani Singida, kutokana na athari za kiafya na kisaikosojia kwa watoto husika, ikiwemo athari za muda mrefu na muda mfupi.

Takwimu za utafiti wa Kidemografia na Afya (TDHS) zinaonesha kuwa kiwango cha ukeketaji wanawake wenye umri wa miaka 15 – 49, kimekupungua kutoka asilimia 18 mwaka 1996 hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2015/16.

Chanzo: habarileo.co.tz