Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vipande 338 vya meno ya tembo vyakamatwa Dar

74299 KIGWAAPIC

Thu, 5 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii nchini Tanzania kwa kushirikiana na maofisa wa Serikali kupitia kikosi cha Taifa cha kuzuia ujangili wamekamata vipande 338 vya meno ya tembo yenye thamani ya  Sh4.40 bilioni.

Meno hayo yalikamatwa jana Jumanne Septemba 3, 2019 eneo la Chamanzi Saku, Dar es Salaam yakiwa wamechimbia chini katika nyumba iliyochukuliwa na mtuhumiwa Hassan Shaban maarufu Nyoni pamoja na wenzake.

Akizungumza wakati akikagua shehena hiyo leo Jumatano Septemba 4, 2019 Waziri wa Wizara hiyo, Dk Hamis Kigwangalla amesema Nyoni alikuwa akitafutwa tangu mwaka 2016.

Amesema ushirikiano ulioonyeshwa na vikosi hivyo vimefanikiwa,  “kumtia mbaroni jangili huyo aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu.Huyu Nyoni amekuwa akikusanya meno ya tembo kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji."

"Amekuwa akihangaika kutafuta meno hayo, kutafuta soko kwa miaka minne bila mafanikio kutokana na wateja kubaki sisi wenyewe.”

Amesema idadi ya vipande hivyo vilivyokamatwa ni sawa na idadi ya tembo 117 waliowindwa ambapo pia kuna meno mawili ya kiboko.

Pia Soma

Advertisement
Amewataja wengine waliokamatwa kuwa ni  Oliva Mchua, Bushiri Lilukena, Haidari Sharifu, Amani Kavishe na Mwita Mara. Amesema kati ya waliokamatwa polisi wapo wawili.

 

Kigwangalla amesema uchunguzi unaonyesha kuna baadhi ya viongozi wa Serikali ambao sio waaminifu wamekuwa wakishiriki ujangili huo, wapo waliokamatwa na wengine kufikishwa mahakamani.

Kigwangalla ametoa siku 30 kwa watu wanaomiliki, kuhifadhi au kufanya biashara ya meno ya tembo kuyarejesha serikalini.

"Natoa wito na huruma kama kiongozi wa kisiasa na Serikali, yoyote mwenye meno ya tembo au kumiliki kuyarejesha serikalini, hatoshtakiwa,” amesema Kigwangalla.

Amesema kwa kushirikiana na vyombo vingine ifikapo mwaka 2024 Tanzania hakutakuwa na biashara ya ujangili kutokana na mipango watakayoiweka ikiwamo kuimarisha jeshi usu.

"Meno tunayoyakamata sasa hivi mengi ni ya kipindi cha nyuma kabla ya utawala wa Rais John Magufuli, kwa sasa tunafikiria kuongeza adhabu zaidi ili ifikapo 2024 kusiwepo tena na biashara hii,” amesisitiza.

Chanzo: mwananchi.co.tz