Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi wa kijiji mikononi mwa Takukuru

28173 Kijiji+pic TanzaniaWeb

Wed, 21 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Viongozi watatu wa kijiji cha Ilindi, kata ya Isuto wilayani Mbeya wanashikiliwa na Takukuru wakituhumiwa kutumia madaraka yao kuwanyanyasa, kuwabambikizia kesi na kuwaweka mahabusu wananchi wanaotoa taarifa za ubadhirifu na udanganyifu katika  ugawaji wa pembejeo za kilimo.

Takukuru huwa haitoi taarifa za mashauri inayoendelea kuyachunguza na ina utamaduni wa kutoa taarifa za watuhumiwa wakati wanapelekwa mahakamani, lakini mkuu wa taasisi hiyo mkoani hapa alisema watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika na kuwaonyesha watuhumiwa hao kwa waandishi wa habari.

Viongozi hao ni Daniel Kahwa, ambaye ni mwenyekiti wa kijiji, Mwalingo Mbenya (ofisa mtedaji) na Timothy Kasekwa ambaye alikuwa katibu wa kamati ya kugawa vocha za pembejeo za kilimo.

Mkuu wa Takukuru wa mkoa, Emmanuel Kiyabo amesema kati ya Oktoba na Novemba walifanya uchunguzi wa vitendo vya ubadhirifu na udanganyifu kwenye ugawaji wa pembejeo za kilimo kwa musimu wa mwaka 2015/2016 maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kufanikiwa kuwakamata watu kadhaa wakiwamo viongozi hao.

Alisema wakati wakiendelea na uchunguzi, walipata taarifa kutoka kwa wananchi wa kijiji hicho kwamba viongozi hao wamekuwa wakitumia madaraka yao kuwanyanyasa, kuwatisha, kuwabambikizia kesi na kuwaweka mahabasu wanakijiji ambao waliotoa ushirikiano kwa Takukuru huku wakijua kufanya hivyo ni kosa.

“Viongozi hawa ambao ni watuhumiwa kwa pamoja na kwa makusudi, kwa kutumia mamlaka ya kiuongozi wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi wa kijiji kile ambao walitoa ushahidi kwa Takukuru, wamefikia hatua ya kuwabambikizia kesi na kuwaweka mahabusu, lengo likiwa ni kulipiza kisasi kwa taarifa walizotoa kwetu huku wakijua kufanya hivyo ni kosa,” alisema.

“Wananchi wa kijiji kile (Ilindi) wameingiwa na hofu kubwa kiasi kwamba wengine wamekimbia makazi yao kwa hofu ya kukamatwa na kubambikiziwa kesi na hawa watuhumiwa. Na taarifa tulizonazo ni kwamba hawa watuhumiwa baada ya kudhaminiwa wamejipanga kwenda kulipiza kisasi kwa wananchi wale.

“Sasa nataka mtambue kwamba pamoja na kesi ya msingi ya ubadhirifu na udanganyifu katika ugawaji wa pembejeo za kilimo, bado mnayo kesi nyingine ya unyanyasaji na natoa onyo endapo mtarejea kijijini na kuendelea na kuwanyanyasa wananchi tutawakamata tena.”

Mbele ya viongozi hao wa Takukuru, watuhumiwa hao waliahidi kwamba hawatarudia kitendo cha kutumia mamlaka yao ya kiuongozi kuwanyanyasa wananchi wao.

“Mkuu ninakuhakikishia sitakwenda kuwanyanyasa wananchi wangu, nitawaongoza kwa kufuata misingi ya sheria na kanuni za uongozi, naomba uniamini katika hili, sitarudia tena,” alisema mwenyekiti wa kijiji hicho.

Naye ofisa mtendaji, Mbenya alisema: “Naapa kwamba sitakwenda kuendelea kuwanyanyasa wananchi wala kuwatishia kwa namna yoyote ile juu ya maisha yao.”

Kauli kama hiyo ilitolewa na Kasekwa aliyesema “nawahakikishia kwamba sitakwenda kumtishia wala kumnyanyasa mwananchi yoyote katika kijiji changu wala kulipiza kisasi”.



Chanzo: mwananchi.co.tz