Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi ushirika matatani rushwa ya Sh.15

6cedae7d7727e308af7964e87816cb69.jpeg Viongozi ushirika matatani rushwa ya Sh.15

Mon, 8 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imebaini kuwapo rushwa ya Sh 15 kwa kila kilogramu ya mazao inayodaiwa kutolewa kwa viongozi wa ushirika wakati wa ununuzi wa mazao na kusema fedha hizo zitawatokea puani. Aidha, serikali imeonya waliotafuna fedha za makusanyo za halmashauri ikisema pia watafikishwa kwenye vyombo vya dola wakati wowote.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, wakati wa ziara ya kikazi ya siku nne ya Rais Samia Suluhu Hassan mkoani Mbeya jana. Bashe alimweleza Rais Samia kuwa Kampuni ya Premium inayohusika na ununuzi wa mazao ya wakulima ina tabia ya kumpa kiongozi wa ushirika rushwa ya Sh 15 kwa kilogramu na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja.

“Nataka nivionye vyama vya ushirika, viongozi saba hawana mamlaka na mazao yenu, nipitie mkutano huu kuwaonya Kampuni ya Premium…,” alisema. Aliendelea kuonya: “Sitasita kuwafutia leseni,… wanapoenda kununua, wanampa kiongozi wa ushirika rushwa ya Sh 15 kwa kilo, ife hiyo tabia, kama una Sh 15 mwongezee mkulima.”

Aliongeza kuwa, “Rais nasema mbele yako kwa sababu najua watakimbilia kwako, hawa watu wamekuwa na tabia ya kumminya mkulima kwenda kumpa bei ndogo halafu wanamalizana na wale viongozi saba wa ushirika kwa kuwapa vichenji vya Sh 15 au 20 kwa kilo.” Bashe alisema tabia ya viongozi wa ushirika kujinufaisha dhidi ya jasho la wakulima imefika mwisho. Pia alisema, Agosti 8 mwaka huu, Rais Samia atashuhudia jumla ya mikataba 21 ya umwagiliaji kusainiwa na kati ya miradi hiyo, 13 itakuwa mkoani Mbeya.

Kwa mujibu wa Bashe, katika mwaka 2021/22, mazao yaliyouzwa nje ya nchi yalikuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.8 kutoka Sh milioni 800 hadi 900 na kati ya fedha hizo, Sh bilioni moja zilitokana na mauzo ya mazao ya chakula.

Kwa upande wake, Dk Mwigulu alisema kumekuwa na baadhi ya wakusanyaji mapato katika serikali za mitaa ambao hugawana fedha hizo na kuzitumia kama zao. Alisema wanakamilisha orodha ya wahusika na watafikishwa kwenye vyombo vya dola wakati wowote kuanzia sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live