Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi CCM wasakwa na polisi kwa kubaka, kulawiti

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawasaka katibu mwenezi wa CCM kata ya Mkolani,  Zephilin Michael (43) na katibu mwenezi wa chama hicho kata ya Buhongwa wilaya ya Nyamagana, Hasan Bushangama (43) kwa tuhuma za kubaka na kulawiti.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna amesema  Michael anatuhumiwa kumlawiti kijana anayekadiriwa kuwa na miaka 16 tukio lililotokea Oktoba 26, 2018  saa 11:30 jioni katika nyumba moja ya kulala wageni iliyopo kwenye kata hiyo.

Kupitia taarifa yake aliyoitoa leo Jumatano Oktoba 31, 2018, Shanna amesema mtuhumiwa alimuajiri kijana huyo kuuza kahawa mtaani kisha alimpangishia chumba katika nyumba hiyo ya kulala wageni ili pindi anapotoka kuuza kahawa awe anafikia hapo.

“Ndipo siku hiyo mtuhumiwa alifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni na kumuuliza mhudumu kama kijana wake yumo ndani ya chumba chake na akaelezwa kuwa yumo, alimfuata humo chumbani huku mhudumu akiendelea na shughuli zake,” amesema.

Amesema baada ya muda mfupi ilisikika sauti ya mtu akipiga kelele kutoka ndani ya chumba hicho na baadaye watu walipochungulia kupitia dirishani walimuona mtuhumiwa akimlawiti kijana huyo.

“Walimtaka afungue mlango lakini aligoma, baadaye alifungua na kutoroka na kisha kijana huyo alitoroka lakini wananchi walitoa taarifa polisi, kwa sasa tunaendelea na msako mkali,” amesema.

Katika tukio lingine la Bushangama, anatuhumiwa kumbaka na kumpatia ujauzito mwanafunzi wa kidato cha pili Sekondari ya Buhongwa mwenye umri wa miaka 17.

Hata hivyo, Shanna amesema mtuhumiwa huyo awali alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi lakini alidhaminiwa na watu wawili baada ya kukamilisha masharti yote ya dhamana Julai, 2018.

Amesema wakati wakiendelea na taratibu za kumfikisha mahakamani walipomuhitaji ndipo walipata taarifa kwamba mtuhumiwa ametoroshwa.

Aliwataja watu waliomdhamini na wakidaiwa kumtorosha ambao kwa sasa wanashikiliwa na polisi kuwa ni Mgassa Carlos (42), mkazi wa Bulele na Jafari Swalehe (57).

Akizungumzia tuhuma za viongozi hao kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Salum Kalli amesema tayari viongozi hao wamevuliwa nyadhifa zao.

Chanzo: mwananchi.co.tz