Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi CCM Ilala wapandishwa kizimbani

48708 Rushwa+pic

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewafikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala vigogo watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ilala wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kuomba rushwa ya Sh 5 milioni na kupokea Sh 3 milioni.

Washtakiwa hao ni Jenifer Mushi ambaye ni Katibu wa CCM Tawi la Amana(47), Devotha Batulake Katibu Kata CCM Ilala (43)na Frank Mang’ati ambaye ni Katibu Hamasa CCM Mkoa wa Dar es Salaam(38).

Wakili wa Takukuru, Veronica Chimwanda aliwasomea mashtaka hayo washtakiwa jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Martha Mpaze.

Chimwanda alidai katika kesi hiyo ya jinai namba 250 ya mwaka huu,kuwa Machi 21,2018 Klabu ya Wazee Amana washtakiwa hao kwa pamoja walishawishi Rushwa ya Sh 5 milioni kutoka kwa Mmiliki wa kampuni ya Daluni East Africa Transport, Daud Kalaghe ili waweze kumpatia kiwanja namba 41 Y kinachomilikiwa na CCM kwa shughuli ya biashara.

Aliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa Machi 22,2018 katika eneo la Msimbazi Sekondari Jenifer alijipatia rushwa ya Sh 3 milioni kwa niaba ya wenzake ili waweze kumpatia kiwanja hicho.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.

Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili Greygori Ngano, Afred Tukio na Mashtaka Charles waliomba washtakiwa wapatiwe dhamana kwa sababu mashtaka yanayowakabili yanadhaminika.

Hakimu Mpaze akitoa masharti ya dhamana alimtaka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili kwenye barua na vitambulisho ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh 5 milioni.

Washtakiwa Devotha na Frank walikamilisha masharti hayo ya dhamana na kuachiwa huru lakini Jenifer alipelekwa rumande kwa kushindwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana.

Hakimu Mpaze ameiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 8,mwaka huu kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Washtakiwa hao walikamatwa Machi 21 baada ya kuwekewa mtego na Takukuru.



Chanzo: mwananchi.co.tz