Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi 24 wasakwa kwa kuuzwa shamba la Serikali

MBARONI.jpeg Viongozi 24 wasakwa kwa kuuzwa shamba la Serikali

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ametoa siku 14 wasakwe na kukamatwa viongozi 24 wanaotuhumiwa kujihusisha kuwatapeli watu na kuwauzia eneo la shamba la mitamba mali ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Viongozi wanaotafutwa ni pamoja na mabalozi, wenyeviti wa mitaa, watendaji walioshirikiana na madalali waliohusika kuwauzia wananchi viwanja katika eneo la shamba hilo lililopo Halmashauri ya Mji Kibaha.

Kunenge alitoa maagizo hayo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Pangani uliowahusisha wataalamu kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha na mkoa kwa ajili ya kutoa msimamo wa serikali kuhusu maamuzi ya eneo hilo ambalo limevamiwa na wananchi kwa ajili ya makazi.

Alisema orodha na majina ya viongozi hao na madalali waliohusika kuwauzia kinyemela wananchi viwanja katika eneo hilo ambalo linamilikiwa na serikali anayakabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na Jeshi la Polisi ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

"Natoa muda wa siku 60 kwa Halmashauri ya Mji Kibaha kupima eneo la shamba hilo namba 34 la mitamba lenye ukubwa wa hekta 4,000 na kubainisha mipaka yote na matumizi yake ili ijulikane kama vile eneo la ujenzi wa ofisi za umma na huduma za kijamii, makazi kabla ya kuanza operesheni ya kuwaondoa wananchi walio ndani ya shamba hilo," alisema Kunenge.

Aliwataka makamanda wa polisi na Takukuru Mkoa wa Pwani kuwahoji viongozi na madalali waliohusika kuwauzia wananchi eneo hilo la shamba namba 34 kinyemela na wachukuliwe hatua za kisheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live