Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Viongozi 20 wa Chadema kortini uhujumu uchumi

Ddaf203c71ebeb961be9e7e7423228c6 Viongozi 20 wa Chadema kortini uhujumu uchumi

Tue, 3 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

VIONGOZI 20 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Singida, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Singida wakikabiliwa na shitaka la uhujumu uchumi.

Mbele ya Hakimu Mwandamizi, Consolate Singano, Mwanasheria wa Serikali aliyeongoza jopo la wanasheria wenzake wawili, Michael Ng’hoboko na Almachus Bagenda, alidai washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu.

Aliwataja washitakiwa hao ni Jingu Jackson, Emmanuel Lissu, Wilson Kidaghoo, Gideon Murya, Steven Mangu, Mika Muna, Joseph Daffi, Swalehe Mangu, Morinyo Muhanja, Benedict John, Salum Kiduka na Ibrahim Madaaka.

Wengine ni Juma Hisu, Lightness Masoud, Mashavu Ibrahim, Ester Kiwali, Debora Shaban, Bahati Sambaa, Christina Hamis na Noela Lemoyani.

Alidai kuwa kati ya Oktoba na Novemba Mosi mwaka huu kwenye maeneo tofauti, washitakiwa huku wakifahamu walishawishi umma kujiingiza kwenye fujo kwa nia ya kuleta machafuko na uasi.

Alitaja shitaka la kwanza kwanza kuwa ni kuongoza genge la wahalifu ikiwa ni kinyume cha Sheria ya Kuhujumu Uchumi Sura ya 200 ya mwaka 2019 Kifungu cha 57 (1) na 60 (2).

Shitaka la pili ni kula njama kwa lengo la kutenda kosa kinyume cha Kifungu cha 385 na 35 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, shitaka la tatu ni kufanya mkusanyiko usiokuwa na kibali kinyume cha Kifungu cha 74 (1) na Kifungu cha 75 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Baada ya kusomewa mashitaka, walikana kutenda makosa hayo na kesi imeahirishwa na itatajwa tena Novemba 13, mwaka huu.

Chanzo: habarileo.co.tz