Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana 50 wakamatwa kwa uhalifu Mwanza

Pingu 1024x769 Wadaiwa kuvunja nyumba na kupora vitu.

Fri, 13 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia vijana 50 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu ikiwepo uporaji, kuvunja nyumba na kupora.

Vijana hao wenye umri kati ya miaka 17 hadi 23 wameunda vikundi tofauti na kuvipatia majina ya “G7, Selebobo, Sanitizer, Barakoa na Covid”.

Taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao imetolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ilemela, Elisante Ulomi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Nyasaka wilayani Ilemela baada ya wananchi katika kata hiyo kueleza kuibuka kwa vitendo hivyo vinavyofanywa na vijana nyakati za usiku.

Ulomi amesema wanaendelea kufanya operesheni maalum dhidi ya vikundi vingine huku akiwataka wazazi kuacha tabia ya kuwaendekeza watoto wao.

​Ametumia fursa hiyo kuwaomba wazazi kuwa na kawaida ya kuwafuatilia watoto wao pale wanaporudi nyumbani na zawadi au vitu vya gharama wawahoji na kuwaonya.

“Watu wanaofanyiwa vitendo hivyo wanafika mahali wanachoka haturuhusu vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na mzazi usilaumu mtu usilaumu Jeshi la Polisi na wananchi wenzako mpaka mtoto anafikia hatua ya kufanya uhalifu maana yake kuna sehemu moja au nyingine hujatimiza wajibu wako,” amesema Ulomi.

Akizungumzia suala hilo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla amesema idadi ya watuhumiwa wa makosa ya uhalifu waliokamatwa wengi wao ni watoto chini ya miaka 18 ambao bado wapo chini ya uangalizi wa wazazi wao.

“Kimsingi hayo ni makundi ya kihalifu na bahati mbaya sana wanaojishughulisha na makundi haya ni watoto wadogo, hii yote ni kwa sababu ya changamoto ya matumizi ya madawa ya kulevya na bangi na kwamba kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama tutahakikisha tunawakamata watuhumiwa wote wanaovunja sheria,” amesema Masalla.

Mkuu huyo wa wilaya amesema vijana au watoto hao wanatoka kwenye jamii na wanawafahamika hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili waendelea kufanya uchunguzi wa chini kwa chini na wawachukulie hatua vijana wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.

"Wazazi ni jukumu letu kulea watoto kwenye maadili pia viongozi wa dini na jamii kwa ujumla, siyo suala la kumuachia mtu mmoja mpaka mtoto anafikia hatua ya kushika panga na kuingia mtaani na kwenda kufanya uhalifu maana yake ni kwamba jamii inayomzunguka jambo hili inakuwa imeshaliona lakini wanashindwa kukemea na kuchukua hatua," amesema Masalla.

Mkuu huyo wa wilaya ameomba ushirikiano kutoka kwa jamii ili kufanikisha kuwakamata watuhumiwa wote anaojihusisha na matumizi na wauzaji wa dawa za kulevya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live