Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana 3 mbaroni mauaji dereva wa bodaboda

631c11794090288bd190bc368f73b1f5.jpeg Vijana 3 mbaroni mauaji dereva wa bodaboda

Thu, 13 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limekamata vijana watatu wakituhumiwa kumuua mwendesha pikipiki ya abiria (bodaboda), Rogers Kessy kwa kumpiga na nyundo kichwani na kumnyonga kwa waya wa kufungia vyuma.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Amon Kakwale alisema jana kuwa, baada ya mauaji watuhumiwa hao waliuweka mwili wa marehemu katika mfuko wa sandarusi na kuutelekeza pembeni mwa barabara ya Moshi/Himo.

Kamanda Kakwale alisema mauaji hayo yalifanywa Mei 11 mwaka huu saa 12:30 jioni eneo la MnaziShah Tours kata ya Kiborlon na kwamba watuhumiwa walikamatwa baada ya Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Sifael Sarun (21) mkazi wa Mnazi, Emanuel Godson (21) mkazi wa eneo la Themanini na Elia Laizer (21) wakazi wa Kibolron katika manispaa ya Moshi.

“Kabla ya mauaji, watuhumiwa walimchukua Kessy na kumwambia anakwenda kubeba meza nyumbani kwa watuhumiwa na walipofika nyumbani alikuta ni meza na wakati anainama kuifungua alipigwa nyundo kichwani kisha wakamnyonga na waya hadi kufa”alisema Kamanda Kakwale.

Alisema baada ya kumuua Kessy, watuhumiwa walipora pikipiki aina ya Toyo yenye namba za usajili MC 880 AYR na kwamba, ilikamatwa nyumbani kwa watuhumiwa kata ya Kiborlon.

Kamanda Kakwale alisema Polisi pia wamekamata watu 30 wanaodaiwa kuhusika na matukio yakiwemo ya kupora mikoba ya wanawake kwa kutumia pikipiki, utengenezaji wa pombe haramu ya gongo na dawa za kulevya.

“Katika msako huu tumekamata pikipiki 8, mitambo 19 ya kutengeneza gongo, mapipa 58 ya kuchemshia pombe hiyo, pombe ya gongo lita 135, dawa za kulevya aina ya heroin kete 25 na bangi misokoto 184” alisema.

Kamanda Kakwale alitoa tahadhari kuwa wananchi wawe waangalifu wakati wa sikukuu ya Idd El Fitr na wasiondoke wote nyumbani kwenda katika ibada kwa kuwa wezi wanaweza kutumia mwanya huo kuiba.

Chanzo: www.habarileo.co.tz