Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigogo wa Zantel, Halotel waikwepa jela, walipa faini

9685 Vigogo+pic.png TZWeb

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vigogo wa kampuni za Zantel na Halotel jana walikwepa kifungo cha miaka saba jela baada ya kufanikiwa kulipa faini ya Sh238 milioni.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kuwaamuru wakurugenzi watendaji wa kampuni hizo, wanaokabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kulipa fedha hizo pamoja na hasara waliyoisababisha ya Sh1.1 bilioni.

Vigogo hao ni mkurugenzi wa Halotel raia wa Vietnam, Le Van Dai (35); mkurugenzi mkuu wa Zantel raia wa Misri, Sherif El Barary; msimamizi wa biashara wa Halotel Zanzibar, Jimmy Mosha (26); Meneja Masoko Halotel, Willy Ndoni (29); Kampuni ya Viettel Tanzania Limited maarufu kama Halotel iliyopo Kinondoni na Kampuni ya Zanzibar Telecomunication PLC maarufu kama Zantel iliyopo Msasani, jijini Dar es Salaam.

Vigogo hao walilipa faini kuepuka kifungo, kasoro washtakiwa Lei Cao na Huang Meng ambao walipelekwa gerezani.

Jana, Hakimu Mfawidhi, Kevin Mhina aliamuru laini za simu walizokamatwa nazo washtakiwa ziteketezwe na vifaa vya mawasiliano vitaifishwe na Serikali.

Pia, aliamuru warejeshewe mali zao binafsi ikiwamo hati zao za kusafiria, hati za ukazi na leseni ya kufanyia kazi.

Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Jacqline Nyantori aliiambia Mahakama kuwa Halotel ni wakosaji kwa mara ya pili. Aliomba washtakiwa hao waadhibiwe kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa kampuni za simu na watu wanaofikiria kufanya makosa hayo.

Chanzo: mwananchi.co.tz