hahidi wa 10 katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, Francis Mrosso ameieleza Mahakama kuwa aliwaeleza Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni na Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Kenani Kihongosi kuhusu suala la Sh90 milioni.
Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana, Mrosso ambaye ni mfanyabiashara amewataja viongozi hao wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali, Tarsila Gervas.
Katika kesi hiyo, Sabaya na wenzake sita, Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya wanakabiliwa na makosa matano ya uhujumu uchumi.
Akitoa ushahidi wake, Mrosso alidai kuwa siku chache baada ya Sabaya na vijana wake kumtishia na kuchukua Sh90 milioni kutoka kwake wakimtisha asipotoa fedha hizo angemfungulia kesi ya uhujumu uchumi, alilazimika kwenda kwa viongozi hao.
Alisema alianza kwenda kwa Kihongosi ambaye kwa wakati huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha na Hamduni aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kulalamikia kulazimishwa kutoa fedha hizo Januari 22, 2021.
Amedai kuwa siku tano baada ya tukio hilo aliendelea kutafakari kitu cha kufanya, kwani alikuwa na woga kwa sababu Sabaya alimwambia watarudi tena, hivyo alienda ofisini kwa Kihongosi kumueleza suala hilo.
“Nilienda kwa Kihongosi kwa sababu aliyekuja kwangu alikuwa mkuu wa wilaya, nikamweleza namna Sabaya alivyokuja ofisini kwangu akiwa na vijana wake akanilazimisha kutoa Sh90 milioni, nilivyomweleza naye akashtuka akachukua simu akataka kumpigia.
“Akaniuliza nina kithibitisho gani, nikamwambia nina slip niliyotolea ile fedha, akaichukua ikatolewa kopi, akajadiliana na wenzake wawili aliokuwa nao pale ofisini, akaahirisha kumpigia akaniambia niache namba za simu kwa kuwa jambo hilo ni kubwa atafikisha ngazi za juu.
“Aliniambia mtu yeyote akinipigia simu akajitambulisha kuwa ni mtu wa usalama nimpe ushirikiano kuhusu atakachoniuliza. Baada ya muda kidogo nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha ni mtu wa usalama, nikamweleza suala lile akaniambia atanirudia ila hakunirudia tena.”
Mrosso alisema katikati ya Februari, alikwenda kwa RPC Hamduni, akamweleza suala hilo ambaye alisema ataitwa kuchukuliwa maelezo na kushauri awe makini sana. Shahidi alisimulia siku moja akiwa katika eneo la kuosha magari kwa Idd, aligongewa kioo na watu wawili na aliposhuka mmoja wao alimweleza Sabaya anamuita.
“Nikashtuka hata gari ninalotumia wanalifahamu, nikaenda hadi alipokuwa na nilipofika alipokuwa Sabaya akaniambia nasikia unanitafuta,” alidai.
Alisema alimweleza kuwa amemshtaki kwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini atanifanya nini?
“Nikamwambia nimekwenda kuangalia fedha zangu alizochukua nitazipataje, Sabaya akaniuliza nikisikia ameteuliwa na Rais kuwa mkuu wa mkoa nitafanyaje?
Alisema baada ya Sabaya kusimamishwa kazi na Rais Samia Suluhu, alipokea barua ya wito kutoka Takukuru wakimweleza suala lake alilotolea malalamiko polisi na kutakiwa kutoa baadhi ya nyaraka, ikiwamo leseni ya biashara, TIN namba na nyaraka nyingine za usajili wa kampuni.
Alipotaka kutoa nyaraka hizo kama vielelezo, mawakili wa utetezi walipinga na Hakimu Mkazi Patricia Kisinda anayesikiliza kesi hiyo akaiahirisha hadi leo kwa ajili ya uamuzi, iwapo vipokewe au la.