Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigogo Rahco wafikisha siku 1,010 mahabusu, upelelezi kesi yao bado haujakamilika

32409 Rahcopic Tanzania Web Photo

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vigogo wawili wa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco) wanaokabiliwa na kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya Dola 527,540 za Marekani wanaendelea kusota rumande kwa siku 1,010  kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Washtakiwa hao ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Rahco, Benhardard Tito, mwanasheria wa zamani  wa kampuni hiyo, Emmanuel Massawe na mwakilishi wa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 14, 2016 kujibu mashtaka nane likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka.

Kuanzia siku hiyo hadi leo Jumatano Desemba 19, 2018 saa 6:00 mchana washtakiwa hao wamefikisha siku 1,010 mahabusu sawa na wiki 144 na siku mbili.

Leo katika mahakama hiyo wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana  na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo, ameieleza mahakama hiyo kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kulipitia.

Ndimbo ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba  wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

“Jalada la kesi hii lipo kwa DPP kwa ajili ya kulipitia na upelelezi wake bado haujakamilika hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” amedai Ndimbo.

Hakimu Simba ameahirisha  kesi  kesi hiyo hadi Desemba 27, 2018 itakapotajwa na kuutaka upande wa mashtaka kufuatilia jalada hilo ili kujua limefikia hatua gani.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015 kwa nia ya kutenda kosa walikula njama kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.

Tito, anadaiwa kuwa Februari 27, 2015 katika ofisi za Rahco zilizopo Ilala alitumia madaraka yake vibaya kwa kuiajiri Kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd kama mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati bila idhini ya bodi ya zabuni ya Rahco.

Tito na Massawe wanadaiwa kuwa Machi 12, 2015 katika ofisi za Rahco Ilala wakiwa katika nyadhifa zao, walisaini barua ya kuihalalisha kampuni hiyo ya Afrika Kusini kuwa mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati na kutoa huduma za ushauri wa kifedha kuhusu mradi huo.

Tito na Massawe wanadaiwa kuwa  Machi 12 na Mei 20, 2015 wilayani Ilala walishindwa kuwasilisha mkataba wa huduma ya ushauri kati ya kampuni hiyo ya Afrika Kusini na Rahco.

Tito na Massawe wanadaiwa Mei 20, 2015 katika ofisi za Rahco, kwa kutumia madaraka yao vibaya walisaini mkataba wa kutoa huduma za ushauri na kampuni ya Afrika Kusini bila ridhaa ya bodi ya zabuni ya Rahco.

Pia, Tito na Massawe wanadaiwa kati ya Mei 20 na Juni 20, 2015 walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kuwasilisha mkataba walioingia na kampuni ya Afrika Kusini kwa mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Tito, Mwinyijuma na Massawe, wanaodaiwa kati ya Machi Mosi na Septemba 30, 2015 katika ofisi za Rahco waliipa kazi kampuni hiyo ya ushauri na kuilipa kwa kutoa huduma za ushauri, malipo ambayo yaliisababishia Rahco kupata hasara ya dola za Marekani 527,540.

Tito anadaiwa Agosti 18, 2015 katika ofisi za Rahco Ilala, kwa kutumia madaraka yake vibaya aliipa kampuni ya ujenzi wa Reli ya China kazi ya kujenga kilomita mbili za reli maeneo ya Soga iliyogharimu dola za Marekani 2,312,229.39 bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya Rahco.

Soma Zaidi: Vigogo Rahco wafikishwa kortini



Chanzo: mwananchi.co.tz