Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigogo KNCU wahofia afya zao kudhoofu

10718 Pic+kncu TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Kudhoofu kwa afya za waliokuwa viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU), kumemlazimu wakili wao kuomba kubadilishiwa tarehe ya kusikilizwa kwa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.

Wakili huyo ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kuwa, badala ya siku ya Jumanne wapangie siku nyingine kutokana na wingi wa mahabusu siku hiyo.

Wakili huyo amesema kutokana na afya za wateja wao kudhoofu, wanapopanda gari la mahabusu lililojaa wataathirika zaidi kiafya.

Viogozi hao wa KNCU na Tanganyika Coffee Curing Company Limited (TCCCo), wanakabiliwa na kesi mbili za uhujumu uchumi na kuisababisha Serikali hasara ya Sh4.9 bilioni.

Washtakiwa hao ni mwenyekiti wa zamani wa KNCU, Aloyce Kitau (70); aliyekuwa makamu mwenyekiti, Hatibu Mwanga (70) na Honest Temba (38) ambaye ni meneja mkuu wa chama hicho.

Wengine ni Maynard Swai (57) aliyekuwa mwenyekiti wa Bodi ya TCCCo na meneja mkuu, Andrew Kleruu (54) ambao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Akiwasilisha ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Bernazitha Maziku jana, wakili wa utetezi Sawayael Shoo aliiambia mahakama hiyo kuwa siku ya Jumanne mahabusu huwa ni wengi mahakamani hapo na hali hiyo huenda ikadhoofisha zaidi afya za wateja wake kwa kuwa hata magari ya mahabusu huwa yamejaa.

“Mshtakiwa wa kwanza na wa pili afya zao ni mbaya sana, hivyo tunaiomba mahakama yako hii tukufu kutubadilishia siku, badala ya Jumanne iwe ni siku nyingine ya wiki kutokana na mahabusu kuwa wengi siku hiyo,” aliomba Sawayael.

Kwa upande wake, wakili mwandamizi wa Serikali, Tamari Mndeme alisema hana pingamizi lolote kuhusiana na ombi la upande wa utetezi na akaiambia mahakama hiyo kuwa, bado upelelezi unaendelea na kuomba wapangiwe tarehe nyingine.

“Mimi sina pingamizi lolote kuhusiana na ombi lililowasilishwa na upande wa utetezi, hivyo ninaomba wapangiwe tarehe nyingine kwani bado upelelezi haujakamilika,” alisema Mndeme.

Hakimu Maziku alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 22.

Chanzo: mwananchi.co.tz