Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vigogo Benki ya Posta jela miaka mitano

14570 Pic+vigogo TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Meneja wa Benki ya Posta tawi la Tabora, Boaz Lunyungu, mhasibu wa benki hiyo na mfanyabiashara maarufu mkoani hapa wamehukumiwa na Mahakama  ya Mkoa wa Tabora kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh100milioni kila mmoja.

Lunyungu pamoja na George Ngatunga (mhasibu) na  Umaiya Makiliga ambaye ni mfanyabiashara walishtakiwa kwa makosa saba, likiwemo la utakatishaji fedha zaidi ya Sh700milioni.

Mbali na adhabu hiyo, baada ya kutiwa hatiani mahakama hiyo imewaamuru washtakiwa hao kulipa Sh710milioni walizoiibia benki hiyo, vinginevyo mali zao zitaifishwe na Serikali kufidia kiasi cha fedha kilichoibwa.

 

Uamuzi wa shauri hilo la jinai namba 154/2015 umetolewa leo Jumatano Agosti 29, 2018 na hakimu mkazi wa mahakama ya Mkoa wa Tabora, Joctan Rushwela, baada ya kuwatia hatiani washitakiwa hao kwa makosa matatu kati ya saba.

Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa muda wa dakika 120, Hakimu Rushwela amesema mashtaka hayo ni kula njama ya kutenda kosa la wizi, kutakatisha fedha pamoja na kosa la wizi.

Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Shedrack Kimaro ulieleza mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Januari 2014 na Julai 2015 katika Benki ya Posta, Tabora.

Wakili Kimaro amedai katika shitaka la kwanza kuwa katika kipindi hicho washitakiwa kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa la wizi.

Amedai kuwa washitakiwa wote watatu katika tarehe tofauti kati ya Januari 2014 na Julai 2015, waliiba Sh710 milioni katika Benki ya Posta tawi la Tabora.

Katika shtaka la tatu linalomkabili meneja na mhasibu huyo, imeelezwa kuwa wakiwa ni watumishi wa Benki ya Posta, walitakatisha fedha Sh710milioni huku wakijua wamezipata kwa njia zisizo halali

Upande wa Jamhuri wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo ulileta mashahidi 16 waliotoa ushahidi na kuthibitisha washtakiwa hao kutenda kosa hilo.

Mbali na hukumu hiyo, washtakiwa hao bado wanakabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi wakiwa na watuhumiwa wengine 13, shauri ambalo bado halijaanza kusikilizwa kwa kuwa jalada lipo kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP).

Chanzo: mwananchi.co.tz