Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vifaa vya ujenzi vyakabidhiwa ujenzi wa bweni Magereza, Shinyanga

Gerezani Imagine Baadhi ya misaada iliyotolewa gerezani hapo.

Wed, 2 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amepokea na kukabidhi vifaa vya ujenzi wa bweni ‘sero’ mpya katika gereza la Wilaya ya Shinyanga maarufu ‘Mhumbu’ vilivyotolewa na wadau mbalimbali ili kukabiliana na uhaba wa malazi unaotokana na changamoto ya msongamano wa wafungwa na mahabusu.

Vifaa hivyo vya ujenzi wa bweni katika gereza la wilaya ya Shinyanga vinatokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Shinyanga ikiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Jasinta Mboneko katika kuondoa changamoto zilizopo kwenye gereza hilo ambalo limeelemewa na idadi ya wafungwa na mahabusu.

Akizungumza wakati wa kupokea na kukabidhi vifaa vya ujenzi wa bweni la Magereza, Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amewashukuru wadau waliojitokeza kuchangia ujenzi huo na kuwaomba wadau kuendelea kujitokeza kuchangia ujenzi wa bweni hilo.

“Kuna msongamano mkubwa wa wafungwa na mahabusu katika gereza hili. Kutokana na changamoto hii tuliwaomba wadau watushike mkono katika ujenzi wa bweni jipya. Tunawashukuru sana wadau mliojitokeza kuchangia ujenzi huu. Tuliwaita na mkaitikia mara moja na tunawaomba wadau wengine wajitokeze, hata kama una matofali 10 wewe tuletee tunayapokea, na sasa kazi ya ujenzi inaanza mara moja”,amesema Mboneko.

Ameeleza kuwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi, bweni hilo jipya litakuwa na uwezo wa kubeba wafungwa na mahabusu 100 na kwamba wanaendelea na jitihada za kutafuta magodoro kutoka kwa wadau wakiwemo GSM kwa ajili ya wafungwa na mahabusu.

Mboneko amewataja miongoni mwa wadau waliojitokeza kutoa michango ya ujenzi wa Bweni katika gereza la Shinyanga ni Kampuni ya Aham Investment Co. Ltd ambayo imechangia matofali 1,000,TANROADS Mkoa wa Shinyanga tripu tano za mchanga na Kampuni ya Jonta Investment Co. Ltd mifuko 100 ya saruji.

Wadau wengine waliokabidhi vifaa vya ujenzi leo ni Kampuni ya Gilitu Interprises Ltd ambayo imechangia shilingi Milioni moja kwa ajili ya nondo na yeye mwenyewe (Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko) akichangia shilingi Milioni moja kwa ajili ya ununuzi wa nondo na wamekabidhi nondo 88.

Wakikabidhi vifaa hivyo wadau hao akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Aham, Ally Ameir, Amina Mikuki kutoka Kampuni ya Jonta Investment Co. Ltd, Mhandisi Mwandamizi kutoka TANROADS Joseph Mayaya na Mkurugenzi wa Kampuni ya Gilitu Enterprises Ltd, Gilitu Makula wameishukuru serikali kuona umuhimu wa kushirikisha wadau katika ujenzi huo wa bweni la magereza kwani serikali pekee haiwezi kumaliza changamoto zilizopo katika jamii.

Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Shinyanga, William Makwaya amewashukuru wadau kwa mchaango wa vifaa vya ujenzi na kwamba mara baada ya kupokea vifaa vya ujenzi shughuli ya ujenzi inaanza mara moja na wanategemea kukamilisha ujenzi huo ndani ya wiki mbili kwani mafundi wamo humo humo gerezani.

Ameeleza kuwa gereza hilo lina uwezo wa kubeba wafungwa na mahabusu wa kiume 130 na wa kike 30 (jumla 160) lakini idadi imekuwa ikipanda hadi kufikia zaidi ya 450 hiyo kusababisha changamoto kubwa ya malazi huku akiomba wadau kuwapatia magodoro kwani yaliyopo ni machache.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live