Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIGOGO WAWILI CWT KORTINI

976b978e83dcf437a9859c940cbad6f9.jpeg VIGOGO WAWILI CWT KORTINI

Tue, 4 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VIGOGO wawili wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kujipatia fedha zaidi ya Sh milioni 13.9.

Washtakiwa hao ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Deus Seif na Mweka Hazina, Abubakar Allawi ambao walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Imani Nitume mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili Nitume alidai kati ya Oktoba 3 hadi Novemba 6, 2018 katika Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa hao wakiwa watumishi wa CWT, walitumia madaraka yao vibaya na kujipatia Sh 13,930,963 kwa manufaa yao wenyewe.

Wakili Nitume alidai kati-

ka shitaka la pili washtakiwa hao kwa kutumia nafasi walizo nazo katika chama hicho walichepusha kiasi hicho cha fedha kwa manufaa binafsi. Washtakiwa hao walikana.

Wakili Nitume alidai upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na kuomba mahakama hiyo iwapangie upande wa mashtaka tarehe ya kusoma maelezo ya awali kwa washtakiwa.

Mshtakiwa Seif aliachiwa kwa dhamana huku Allawi akipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwasilisha mahakamani fedha taslimu Sh 3,487,400 pamoja na kupeleka mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh milioni saba.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 17, mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hoja za awali.

Awali kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Takukuru, ilieleza kuwa washtakiwa hao walikuwa wakichunguzwa na taasisi hiyo na uchunguzi ulibaini kuwa mwaka 2018 walitumia kiasi hicho cha fedha mali ya CWT kugharamia safari ya kwenda Ivory Coast kuhud-

huria mechi ya mpira wa miguu baina ya Taifa Stars na timu ya taifa ya Ivory Coast.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa fedha hizo zilitumika kununua tiketi za ndege na kulipia gharama za malazi nchini humo.

Katika hatua nyingine, mkazi wa Uwanja wa Ndege Dar es Salaam, Kuluthumu Tunku, amefikishwa katika mahakama hiyo akikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 242.

Mshitakiwa huyo alifikishwa na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Ruboroga.

Akisoma mashtaka kwa mshtakiwa, Wakili wa Serikali Sylivia Mitanto alidai Februari 17, 2020 katika eneo la Upanga jijini Dar es Salaam mshtakiwa huyo alikutwa akisafirisha dawa hizo za kulevya.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 17, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz