Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Walimu ‘waukimbia’ msiba wa mwanafunzi aliyejiua Moshi

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wakati mwili wa mwanafunzi Emmanuel Tarimo aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Rau, ukizikwa jana kijijini kwao Kitowo, Rombo-Mashati, hakuna mwalimu aliyehudhuria msiba huo.

Emmanuel aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha nne alijinyonga hadi kufa Septemba 4 kwa kutumia tai saa chache baada ya kuhojiwa na walimu akituhumiwa kumpa mimba mwanafunzi mwenzake.

Wakati mamia ya wanafunzi na wakazi wa eneo hilo wakihudhuria msiba huo, jana alionekana mwalimu mmoja ambaye hata hivyo alisema amefika kama mmoja wa ndugu wa familia ya marehemu.

Ndugu huyo, Allen Mushi, yupo katika shule hiyo akiwa kwenye mafunzo kwa vitendo.

Akizungumza na Mwananchi, Mushi alisema ameguswa na msiba huo kwa sababu alimfahamu Emmanuel tangu akiwa mdogo na yeye ni ndugu wa karibu wa familia hiyo.

“Nimepokea msiba huu kwa masikitiko makubwa kwa sababu ya aina ya kifo,” alisema huku akisisitiza kuwa hawakufika kuiwakilisha shule, bali alikwenda kama ndugu.

Bibi wa marehemu, Felista Wilbard alisema wanashangazwa kutouona uongozi wa shule na kuwaongezea mashaka juu ya kifo cha mtoto wao.

“Uongozi haujafika hapa kutoa pole na ndiyo maana tunaona ipo sababu imejificha,” alisema.

Mjomba wa marehemu, Emmanuel Mosha alishangazwa na namna tukio hilo lilivyoitenganisha shule hiyo na familia yao.

“Sijaelewa kwa nini walimu wamesusa msiba huu kwani walikuwa na ugomvi na ndugu yetu?” alihoji Mosha.

Wakati huohuo, mwenyekiti wa mtaa wa Sabasaba, Kijiji cha Rau, William Kiria alinusurika kupigwa na wanafamilia ya Tarimo wakati akitoa salamu za rambirambi msibani hapo. Katika salamu zake, Kiria alisema ametumwa kuuwakilisha uongozi wa shule ya Rau.

“Tunashangaa kwa nini mwili ulining’inia kwenye kamba kwa saa nne, kwa nini?” alisema Kiria.

Kauli hiyo ndiyo iliyowanyanyua wanafamilia ambao walimkunja shati na kutaka kumpiga hali iliyosababisha aondolewe msibani hapo.

Awali, wakati mwili wa Emmanuel ukiagwa nyumbani kwa mama yake mdogo katika mtaa huo, mama wa marehemu, Amina Maro alipoteza fahamu kwa saa kadhaa wakati akimuaga mwanawe.

Wanafunzi wengi walimiminika msibani hapo na baadhi walitumia usafiri wa bodaboda kwenda kumzika mwenzao kijijini kwao Kitowo, Rombo- Mashati.

Chanzo: mwananchi.co.tz