Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Polisi yafungua jalada mwandishi kupigwa na askari, wadau waja juu

Video Archive
Sat, 11 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro akiagiza kufunguliwa kwa majalada mawili kuchunguza tukio la mwandishi wa habari kupigwa na askari wake, wanahabari, wanaharakati na wanasheria wamekuja juu wakihoji utendaji kazi wa jeshi hilo.

Jana, video inayoonyesha mwandishi huyo, Silas Mbise wa Radio Wapo akipigwa na askari kadhaa wa polisi iliwaibua ilisambaa kwenye mitandao ya jamii na kuzua mjadala.

Iliwaonyesha askari Polisi waliovaa sare za jeshi hilo wakimpiga mwandishi huyo aliyekuwa kifua wazi akiwa ameketi na kisha kuendelea kumpiga hata baada ya kuwa amelala kifudifudi katika moja ya vyumba vya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Agosti 8 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Simba (Simba Day).

Akizungumzia suala hilo jana, msemaji wa Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema IGP Sirro ameagiza kufanyika uchunguzi wa tukio hilo na kwamba yamefunguliwa majalada mawili ya uchunguzi akisema licha ya mwandishi huyo kupigwa naye anadaiwa kumshambulia askari.

Alidai kwamba Mbise anatuhumiwa kufanya fujo uwanjani hapo ndipo polisi walipomdhibiti na kwamba kama atapatikana na hatia atachukuliwa hatua.

“Polisi naye anadaiwa kumpiga Mbise, jalada la uchunguzi linafunguliwa, akipatikana na hatia naye atapelekwa mahakamani, hakuna aliye juu ya sheria,” alisema.

Aliwataka waandishi wa habari wasilichukulie suala hilo kama ni ugomvi baina yao na polisi.

“Niwaombe waandishi wa habari wajue kuwa jeshi la polisi linafanya kazi kwa weledi na uhuru wa sheria. Polisi wanapodhibiti watu basi yule nayejifanya mjanja ndiye anadhibitiwa na polisi wanatakiwa kuzingatia taaluma, mtu akifanya fujo si lazima apigwe,” alisema.

Aidha, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema polisi wameanza uchunguzi wa tukio hilo baada ya kuona video.

“Tayari jeshi la polisi limefungua jalada la uchunguzi kuhusiana na tukio hili ili kubaini ukweli na tayari askari waliokuwa zamu eneo la tukio wameanza kuchunguzwa ikiwamo wawili kuhojiwa” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema jukumu la polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao na si kuwapiga raia waliotenda kosa ambao hawajakataa kutii sheria ya kukamatwa.

Tukio hilo lilitokea sambamba la mwandishi mwingine wa habari wa Tanzania Daima, Sita Tuma ambaye alikamatwa na kuwekwa rumande kwa saa kadhaa wakati alipokuwa akifanya kazi kwenye mkutano wa kampeni za udiwani za Chadema.

Katika ukurasa wake wa Facebook, Mbise ameandika ujumbe kwa maandishi makubwa akisema hawezi kuisahau siku hiyo kwa kipigo alichokipata wakati akitekeleza majukumu yake ya kikazi.

“Sitasahau siku ya Agosti 8 Uwanja wa Taifa, umesimama unapigwa, umekaa chini umepigwa, umelala umepigwa sasa sijui walitaka nipigane nao, kisa hatutakiwi kuingia kwenye press wakati tumevaa na kitambulisho. Kwani mkiongea hamueleweki hadi mpige? Au kama kuna hatari ya usalama kuna onyo lolote mlitoa?”

Alisema si mara ya kwanza kwa waandishi wa habari kukutwa na jambo hilo lakini imani yake ni kwamba vitendo hivyo vinafanywa na askari wachache wa Jeshi la Polisi wasiojua wajibu wao.

Mkurugenzi wa Radio Wapo, Barikiel Gadiel alisema licha ya tukio hilo, hawana mpango wa kushtaki, bali kuzungumza na uongozi wa Jeshi la Polisi.

“Tunafuatilia kuhakikisha haki inatendeka, ila hatuna mpango wa kwenda kufungua kesi mahakamani, tunataka tukazungumze na wakubwa wa Polisi. Kwa sababu wale waliompiga ni askari wa chini,” alisema Gadiel.

Maoni ya wadau

Lakini wakati Gadiel akisema hayo, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume alisema kitendo hicho ni uvunjifu wa sheria na kwamba chama chake kipo tayari kufungua mashtaka kama Mbise atawapa ushirikiano.

“Polisi hawana haki ya kupiga watu. Nimeiona video ile, yule mtu hakuwa na upinzani wowote kwa askari wale, lakini waliendelea kumpiga mateke ya kichwa na mbavuni. Kilichonishtua ni kuona unyama mkubwa kama ule ukifanyika nchini,” alisema Karume.

“TLS tunaweza kumsadia kisheria, lakini ni lazima yeye mwenyewe alalamike, maana haiwezekani kuwe na kesi bila mlalamikaji...”

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Jesse Kwayu alisema polisi hawana mamlaka ya kumpiga yeyote kwani kazi yao ni kukamata na kufungua mashtaka ili madai na tuhuma zinazomkabili zikathibitishwe mahakamani.

“Vitendo hivi vinakandamiza uhuru wa habari na wa wananchi kwani wanahabari wanafanya kazi hiyo kwa mujibu wa sheria,” alisema, “Tunamwambia Mkuu wa Jeshi la Polisi awaambie polisi wake kuwa wanatumia mabavu na hizi ni njama za kuzuia waandishi wa habari kufanya kazi yao, na ni uvunjaji wa haki za msingi za wananchi kupata habari.”

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema wanalifuatilia suala hilo pamoja na matukio mengine ya uvunjifu wa haki za binafamu na watataoa tamko mwisho wa wiki.

Akizungumzia suala hilo, Wakili maarufu, Harold Sungusia alisema Tanzania inapitia kwenye tatizo kubwa la kutokuwapo kwa utawala wa sheria.

Aliongeza: “Kuna watu wengi tu wanapigwa na kuteswa, haki za binadamu zinavunjwa, lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.”

Nahodha wa timu ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta pia amezungumzia tukio hilo katika ukurasa wake wa Twitter; “Sio kitendi cha kiungwana askari kupiga mwandishi katika eneo la michezo, mpira ni mchezo unaoleta amani sio kuvunja amani.”

Chanzo: mwananchi.co.tz