Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mwanafunzi ajinyonga baada kutuhumiwa kumpa mimba mwenzake

15926 Ajinyonga+pic TanzaniaWeb

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Rau mjini Moshi, Emmanuel Tarimo (18), amejinyonga hadi kufa baada ya kuhojiwa kwa saa 12 na jopo la walimu juu ya tuhuma za kumpa ujauzito mwanafunzi mwenzake.

Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alihojiwa na walimu wake juzi asubuhi hadi jioni akishinikizwa kukiri kufanya kitendo hicho, lakini aliwajibu kuwa hahusiki.

Akizungumzia tukio hilo jana, mkuu wa shule hiyo, Nyoni Njinjinji alisema mwanafunzi huyo baada ya kukana tuhuma hizo kwa mdomo alielekezwa na mwalimu wake wa nidhamu kuandika barua na alitekeleza agizo hilo.

“Kwenye barua aliyoiandika alikana tena kuwa hana uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi mwenzake huyo wa kidato cha kwanza,” alisema Njinjinji. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema mwanafunzi huyo alijinyonga akiwa katika sebule ya nyumbani kwao kwa kutumia mkanda wa suruali yake.

“Usiku wa kuamkia Septemba 4 (juzi) saa tano usiku mwanafunzi huyo alikutwa amejining’ia nyumbani kwao akiwa ameshakufa.

“Baada ya kufuatilia kujua nini kilimsibu hadi kujiua, inaonekana baada ya walimu wake kumuita kwa mahojiano kumuuliza kuhusu tuhuma za kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi mwenzake kitendo kile kilionekana kilimfedhehesha sana, ndiyo maana alichukua uamuzi wa kujinyonga,” alisema Kamanda Issah.

Barua ya mwanafunzi wa kike

Mbali ya Emmanuel, walimu hao pia walimhoji msichana anayetuhumiwa kupewa mimba na pia kumtaka kuandika barua. Katika barua yake, mwanafunzi huyo alidai kuwa Agosti 29 akiwa na Emmanuel katika chumba cha mwalimu aliyemtaja kwa jina moja la Kyra walifanya mapenzi, jambo ambalo mvulana alilikanusha kwenye barua yake akisema alikuwa na uhusiano na msichana mmoja anayesoma Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Muco).

Hata hivyo, inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo wa kike awali alikuwa akisambaza taarifa shuleni hapo kuwa ana mimba ya Emmanuel, taarifa ambazo ziliwafikia walimu ambao waliagiza matroni awapeleke wanafunzi wote kupimwa hospitali, lakini baada ya vipimo, binti huyo hakuonekana kuwa na ujauzito.

Baada ya mahojiano

Mwalimu Njinjinji alisema baada ya Emmanuel kumaliza kuhojiwa, alielekea nyumbani, “Lakini asubuhi nilipigiwa simu na mwenyekiti wa kijiji akinipa taarifa ya mwanafunzi huyo kujinyonga.”

Alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho kwa sababu hawakutarajia kama angeweza kuchukua uamuzi mgumu kiasi hicho.

Familia yazungumza

Wakati mkuu huyo wa shule akisema hayo, ndugu wa mwanafunzi huyo waliozungumza na Mwananchi jana, waliulalamikia uongozi wa shule kwa kitendo cha kumlazimisha mtoto wao kukiri kumpa ujauzito mwanafunzi mwenzake wakisema hawakumtendea haki.

Dada wa marehemu, Teddy Maro alidai kuwa ndugu yao alitishwa na walimu hao hali iliyomjengea hofu hadi kuchukua uamuzi wa kujinyonga. “Ndugu yetu alipewa vitisho kutoka kwa walimu ndiyo maana alichukua hatua ya kujiua, tunaomba Serikali ichunguze hili tukio, kwanza limetupa fedheha kubwa kama familia,” alisema Teddy.

“Hata kama alifanya kosa ilitakiwa wazazi wapewe taarifa ndipo hatua ya kumhoji ingefuata.”

Babu wa mwanafunzi huyo, Jerome Maro aliiomba Serikali iwafuatilie walimu hao kutokana na vitisho ambavyo inadaiwa walivitoa kwa mwanafunzi. “Nimesikitishwa sana na tukio hili, ninaiomba Serikali ifuatilie walimu waliohusika kutoa vitisho kwa mtoto wetu hadi kujiua,” alisema.

Mwanafunzi mwenzake

Akizungumzia tukio hilo, Erick Mshanga aliyekuwa akisoma darasa moja na Emmanuel alisema hatua aliyoichukua mwenzao imewaumiza.

Alisema hakupaswa kuchukua hatua hiyo na badala yake angewashirikisha wenzake wampatie mawazo ya nini cha kufanya.

Mwili wa mwanafunzi huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Mawenzi na anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwao Mashati Rombo.

Chanzo: mwananchi.co.tz