Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Anayedaiwa kutaka kumzamisha mwanaye mtoni kuchunguzwa akili

Video Archive
Sat, 21 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema wanashirikiana na madaktari wa kitengo cha afya ya akili kumchunguza, Benson Bernard (31) anayedaiwa kutaka kumzamisha mtoni mwanaye, Goodchance mwenye umri wa miaka saba.

Mutafungwa ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 21, 2019 katika mkutano na waandishi wa habari wakati akizungumzia tukio hilo lililotokea juzi Alhamisi Desemba 19, 2019 saa 12 jioni katika maporomoko ya maji ya mto Morogoro eneo la Nguzo Campsite.

Amesema mkazi huyo wa Kihonda akiwa na mwanaye anayesoma shule ya awali ya Ebenezer, walikutwa wakiwa watupu huku mtuhumiwa akiwa ameshika panga na msumeno.

Mutafungwa amesema walipata taarifa kutoka kwa raia wema waliomtilia shaka mtuhumiwa huyo.

Amesema walipofika walimtaka atoke kwenye maji lakini alikaidi maagizo hayo na kuanza kuzungumza lugha isiyoeleweka huku akizidi kwenda kina kirefu kwa lengo la kumzamisha mtoto huyo.

Amebainisha kuwa askari walijitosa kwenye maji na kuanza kumvuta, “walifanikiwa kumchukua mtoto, kumkamata baba ambaye anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi. Mtoto yupo kwa mama yake.”

Mama wa mtoto huyo, Mary Shao amesema mumewe alianza kuwa na tabia na mwonekano ambao hakuuzoea kuanzia Novemba 29, 2019.

“Alikuwa akiongea mambo yasiyoeleweka, nashukuru kuona hali ya mtoto wangu ni nzuri,” amesema Mary akibainisha kuwa kabla ya tukio hilo hakuwa na ugomvi na mumewe.

Amesema siku ya tukio Bernard alimchukua mtoto kwa maelezo kuwa wanakwenda kuogelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz