Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Aliyefia mikononi mwa polisi azikwa

Video Archive
Wed, 3 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi/Dar. Mwili wa Henry Kiwia, dereva wa daladala za Kiborlon aliyefariki dunia baada ya kuwekwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi umezikwa jana huku ndugu wakitaja mambo mawili wanayodai yana utata juu ya kifo cha ndugu yao.

Kaka mkubwa wa marehemu, Hudson Kiwia alieleza hayo jana katika kikao cha ukoo muda mfupi baada ya kutoka kuzika.

Akisoma taarifa ya uchunguzi wa kifo cha Henry kufuatia uchunguzi wa kifo chake uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na daktari kutoka jijini Arusha, alisema ilibainika kuwa alinyongwa na kitu chenye mfano wa waya na alikutwa akiwa na nguo ambazo si zake.

Siku mbili zilizopita mwili huo ulichukuliwa na polisi na ndugu hao kutoka Hospitali ya Mawenzi na kupelekwa KCMC kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Alisema utata wa kwanza unatokana na taarifa ya polisi kuwa ndugu yao alijinyonga kwa suruali ya ‘jeans’ wakati daktari huyo amesema alinyongwa na kitu mfano wa waya.

“Kwamba alijinyonga kwa kutumia suruali ya jeans si kweli maana mwili wake ulikutwa na alama kwenye koo na jeraha huku akiwa amevalishwa bukta nyeusi haikuwa yake,” alisema Hudson.

“Katika taarifa ambayo tumepewa na daktari imesema kuwa ndugu yetu hakupigwa kabisa na badala yake alinyongwa kwenye koromeo na kitu chembamba ambacho kinadhaniwa kuwa ni waya, alikosa pumzi na kusababisha kifo chake.”

Polisi wafafanua

Alipoulizwa kuhusu madai hayo ya familia ya marehemu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Isah alisema, “ndugu yangu huyo anayesema (Henry) amenyongwa ni afadhali akaulizwa yeye..., hapo kulikuwa na utata na walikutanishwa (ndugu) wote na ukafanyika uchunguzi. Ndugu waligomea hata kuchukua maiti, lakini kama yeye(daktari) anasema hivyo ni yeye ndiyo kasema, taarifa iliyotolewa (awali) haikusema amenyongwa, sisi tunachojua alijinyonga.”

Alipoulizwa kuhusu ukweli wa taarifa ya daktari alisema, “sasa nyinyi Mwananchi ndiyo huwa tunakosana hapo kwa sababu utasikia kamanda kaibua utata. Sasa ni bora kukaa kimya tu kwa sababu suala hili limeshakuwa na mtazamo tofauti. Sisi tulifanya kazi kwa kushirikisha watu wote, kama huyo mwingine anaamua kulianzisha...taarifa iliyotolewa imeshatolewa na imeenda vizuri kwa wananchi,”

Ibada ya mazishi

Katika ibada ya mazishi iliyoongozwa na mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kiborlon, Mchungaji Sulemani Maro alisema japo familia hiyo imepata pigo na jeraha kubwa maneno ya Mungu ndio yatakayowafariji.

“Najua familia hii ina maswali mengi kuhusiana na tukio hili la kumpoteza mtoto wao mpendwa lakini hii inatokana na watu kupoteza upendo na kufanya mambo ya kinyama na ndio yanayopelekea mambo haya,” alisema mchungaji huyo

Mwenyekiti wa waendesha Hiace mkoani Kiimanjaro, Cathbert Temu alisema kuwa msiba huo umewagusa na kuwasikitisha kwa kuwa sababu za kifo cha mwenzao hazieleweki.

“Tunaomba polisi waliohusika na mauaji haya wachukuliwe hatua za kisheria kwani sisi tunaamini polisi ni sehemu salama yenye kulinda raia na mali zake kwa kweli hii inaumiza sana kwani tulipofuatilia jambo hili tulipewa taarifa ambazo haziridhishi,” alisema Temu.

Ilivyokuwa

Inadaiwa kuwa Henry alikamatwa akiwa na mwenzake Obasanjo Kitwi, jirani na Stendi ya Kibprlon Ijumaa ya Septemba 21 saa 5:00 asubuhi na polisi waliokuwa doria na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Wilaya.

Kamanda Isah alikaririwa akisema kuwa usiku wa Septemba 23, marehemu aliwehuka akiwa mahabusu na kuanza kumwaga maji hali ambayo alidai iliwalazimu polisi kuwahamishia eneo lingine mahabusu wenzake wote na kumuacha peke yake, na ndipo alipogundua amejinyonga kwa kutumia suruali yake ya jeans.

Kauli hiyo iliwakera wanafamilia na kuamua kususia mwili huo hadi utakapofanyika uchunguzi wa kina kujua sababu za kifo cha ndugu yao, wakidai kuwa alikufa kutokana na kipigo cha polisi

Mama wa marehemu, Jaikamesia Kimambo alidai kuwa siku mwili wa mwanaye ulipotolewa mahabusu, polisi waliwafukuza hapo kituoni kitendo kilichoashiria kwapo kwa nia ovu.

Chanzo: mwananchi.co.tz