Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utoroshaji makontena 329 kesi iliyoweka rekodi Mahakama ya Mafisadi

49797 Pic+makontena

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Machi 27 mwaka huu, Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya mafisadi, iliwahukumu adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela, washtakiwa wawili na mmoja kifungo cha miaka miwili jela katika kesi ya makontena yaliyotoroshwa bandarini.

Mbali na adhabu ya kifungo, pia mahakama hiyo iliwaamuru wote kwa pamoja kuilipa Mamlaka ya Mapato (TRA), fidia ya Sh6.35 bilioni ikiwa ni nusu ya hasara waliyoisababisha kwa kutorosha makontena 329 katika Bandari Kavu ya Azam (AICD), bila kulipiwa kodi.

Hii ni kesi ya kipee kutokana na mambo mbalimbali. Kwanza ni kutokana na aina ya makosa ya washtakiwa, pili ni namna makosa hayo yalivyoibuliwa na washatakiwa kutiwa mbaroni hatimaye kufunguliwa mashtaka.

Mambo mengine ni washtakiwa waliohusishwa katika kesi hiyo tangu mwanzo hasa aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza kuvuma sana katika vyombo vya habari na hata mitaani.

Kubwa zaidi ni kwamba hii ndiyo kesi iliyoweka rekodi ya kufungua pazia la Mahakama ya Ufisadi kwa kuwa ni ya kwanza ya ufisadi kufunguliwa katika mahakama hiyo katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi na hata kutolewa hukumu.

Jinsi uhalifu ulivyoibuliwa

Novemba 27, 2015, ikiwa ni siku nane tu tangu Kassim Majaliwa alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Novemba 19 na kuapishwa kesho yake, alifafanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam.

Kupitia ziara hiyo, Majaliwa alibaini kuwa katika kumbukumbu za Mamlaka ya Bandari (PTA) kuna taarifa ya makontena 349 yenye thamani ya sh80 bilioni, lakini taarifa hizo hazipo kwenye kumbukumbu za TRA.

Alipomuuliza Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade kuhusiana na upotevu wa makontena hayo bila kulipiwa kodi, alikiri kuwepo kwa upotevu na kwamba walifanya ukaguzi kwenye ICD moja na kukuta makontena 54 yamepotea kwa njia ya wizi.

Aliongeza kwamba walipoendelea na ukaguzi makontena yaliongezeka na kufikia 327 na kwamba wanaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), huku akiongeza kwamba mmiliki wa ICD hiyo ametakiwa kulipa faini ya Sh12.6 bilioni na alikuwa ameshalipa Sh12.4 bilioni.

Alipoulizwa kama ana majina ya watumishi wanaohusika katika wizi huo hakutoa jibu la moja kwa moja na badala yake alisema anayo na akaomba Waziri Mkuu ampe muda wa kuyatafuta.

Wakati kamishna huyo akiomba apewe muda, kumbe Waziri Mkuu tayari alikuwa na orodha yao, aliyatoa na kumuonyesha orodha ya makontena yaliyopotea mpaka namba za magari ambayo yalitumika kuyabeba, hivyo Bade hakuwa na jinsi badala yake alikiri kuwa ni ya kweli.

Akatangaza kuwasimamisha kazi maofisa watano na watumishi watatu wa TRA kutokana na upotevu wa makontena hayo.

Waliosimamishwa kazi ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki; Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya; Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Haruni Mpande; Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara wa TRA, Hamisi Ali Omari na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD), Eliachi Mrema.

Pia, alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kuwakamata ili kusaidia polisi katika uchunguzi, kuzuia hati zao za kusafiria na kuchunguza mali zao kuona kama zilikuwa zinaendana na kipato chao cha utumishi wa umma.

Vilevile aliwaagiza Kamishna Bade na naibu wake, Lusekelo Mwasena, wahakikishe wanashirikiana na polisi kufuatilia upotevu huo na kwamba fedha hizo zinapatikana na zinarudi serikalini.

Wanane waliotiwa mbaroni kizimbani

Wiki moja baada ya ziara na kutolewa kwa maagizo ya Waiziri Mkuu dhidi ya watuhumiwa wa makontena hayo, Desemba 4, 2015, watuhumiwa wanane walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mawili kuhusiana na utoroshwaji wa makontena hayo.

Waliopandishwa kizimbani siku hiyo ni Masamaki, Mponezya, Meneja Usimamizi na Ufuatiliaji wa Forodha, Burton Mponezya na Mrema.

Wengine ni Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara TRA, Hamis Ally Omary; Meneja wa Oparesheni za Usalama na Ulinzi ICD, Raymond Louis; Mkuu wa AKitengo cha Tehama TRA, Haroun Mpande na Meneja wa Azam (AICD), Ashrafu Khan.

Wote walisomewa mashtaka mawili ya kula njama kuidanganya Serikali na kuisababishia hasara ya Sh12.7 bilioni.

Walidaiwa kuwa kati ya Juni Mosi na Novemba 17, 2015 walikula njama kwa kuidanganya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa makontena 329 yaliyokuwapo katika Bandari Kavu ya Azam yalitolewa baada ya kodi zote kufanyika huku wakijua si kweli.

Katika shtaka la pili, walidaiwa kuwa katika kipindi hicho jijini Dar es Salaam, kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 12.7 bilioni.

Kesi hiyo ilivuta hisia za umma na kusababisha jina la mshtakiwa wa kwanza (Masamaki) kutajwa sana katika kona mbalimbali za jiji la Dar es Salaam, huku akihusishwa na umiliki wa mali nyingi zikiwamo nyumba 70, tuhuma ambazo haijulikani nani alizianzisha.

Masamaki na wenzake wafutiwa mashtaka

Hata hivyo, baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika, Julai 13, 2017, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) aliwafutia mashtaka Masamaki, Mponezya (Habib) Mponezya (Burton), Mrema na Khan na kuachiwa huru huku kesi ikiedelea kwa Omary, Louis na Haroun Mpande.

Baada ya kuwaondolea mashtaka Masamaki na wenzake, upande wa mashtaka uliwaongeza washtakiwa wengine wanne akiwamo, Khalid Yusuph Hassan na Benson Malembo, ofisa wa kampuni ya uwakala ya Regional Cargo Service Ltd, iliyohusika na uondoaji wa makontena hayo.

Wengine walioongezwa ni David Faustine Chimomo na Safina Kassim Rupia, wote wa AICD, kisha wakasomewa mashtaka mapya 110.

Katika ya mashtaka hayo, 105 yalikuwa ya kughushi nyaraka mbalimbali kuhusiana na makontena yaliyotoroshwa, na mashtaka mengine yalikuwa ya utakatishaji fedha, ukwepaji kodi na kuisababishia TRA hasara ya Sh12.7 bilioni.

Wakati kesi hiyo ikiendelea Mahakama ya Kisutu ili kukamilisha taratibu za awali ukiwamo upelelezi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu kuanza kusikilizwa, harakati za uanzishwaji wa Mahakama ya mafisadi, ambayo ilikuwa ni ahadi ya Rais John Magufuli, nazo zilikuwa zikiendelea.

Mahakama hiyo ilikuwa ni moja ya ahadi kubwa za Rais Magufuli wakati wa kampeni zake mwaka 2015 kama hatua ya kupambana na rushwa kubwa na ufisadi nchini.

Hatimaye uanzishwaji wake ulikamilika na ikawa tayari kuanza majukumu yake, mwaka 2016, ikiwa imeanzishwa kama Divisheni ya Mahakama Kuu yenye dhamana ya kushughulika na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

Mahakama hiyo ilipewa jina la Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Kwa mujibu wa sheria iliyoianzisha mahakama hiyo, makossa yanayostahili kupelekwa mbele yake ni ya rushwa na uhujumu uchumi yenye thamani ya kuanzia Sh1 bilioni na kuendelea.

Hata hivyo, sheria hiyo inampa DPP mamlaka ya kupeleka kesi huko hata kama thamani ya fedha inayohusishwa haifiki kiasi hicho iwapo ataona kuna umuhimu wa kuipeleka huko.

Miezi kadhaa baada ya kukamilika kwa mahakama hiyo hakukuwa na kesi kubwa ya ufisadi iliyofunguliwa, baadhi ya watu wakaanza kusema kuwa mahakama hiyo imekosa washtakiwa.

Wengi walidhani mtuhumiwa wa ufisadi akishakamatwa tu anapelekwa huko moja kwa moja la hasha. Ni sharti kwanza kesi hiyo ifunguliwe katika mahakama ya chini kama mahakama ya wilaya au ya hakimu mkazi kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali ikiwa ni pamoja na upelelezi.

Baada ya hatua hizo ndipo kesi hiyo huhamishiwa huko kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi na hatimaye kutolewa hukumu.

Wakati upelelezi wa kesi ya makontena unakamilika, kesi hiyo ilifungwa rasmi katika Mahakama ya Kisutu na kuhamishiwa mahakama ya mafisadi kwa ajili ya usikilizwaji kamili na uamuzi kwani tayari mchakato wa kuianzisha ulikuwa umeshakamilika na kuwa tayari kwa kazi.

Kesi hiyo ilihamishiwa mahakamani hapo mwaka 2017 na kupewa usajili wa kesi namba 01 ya mwaka 2017, hivyo ikaweka rekodi ya kuwa kesi ya kwanza kufunguliwa mahakamani hapo kwa ajili ya hatua ya usikilizwaji na uamuzi.

Kabla ya kesi hiyo kulikuwa na kesi nyingine ambazo tayari zilikuwa zimeshapelekwa mahakamani hapo, hata hivyo, zilikuwa zinahusu maombi ya dhamana tu na si usikilizwaji wa kesi ya msingi kama hii.

Kuna kesi nyingine ambazo zilikuwa zimeshasikilizwa na hata kutolewa hukumu katika mahakama hiyo, lakini hizo ni za dawa za kulevya.

Kesi hiyo ilisikilizwa na Jaji Winfrida Korosso, ambapo upande wa mashahidi uliwaita jumla ya mashahidi 85 na miongoni mwao ni wale waliokuwa washtakiwa waliofutiwa mashtaka na DPP katika Mahakama ya Kisutu, Masamaki na Khan aliyekuwa meneja wa Azam ICD.

Hawa baada ya upelelezi kukamilika upande wa mashtaka ulibaini kuwa walipaswa kuwa mashahidi muhimu kwa upande wao, ndio maana ukawaondoa katika mashtaka na kuwafanya kuwa mashahidi.

Baadhi ya mashahidi na ushahidi wao

Kwa mujibu wa mmoja wa mawakili wa Serikali waliokuwa wakiendesha kesi hiyo, Masamaki ndiye aliyebaini uwepo wa utoroshwaji wa makontena hayo kama ilivyoelezwa na aliyekuwa Kamishna Mkuu, Bade mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa siku ile ya ziara yake ya kushtukiza.

Khan aliyekuwa shahidi wa kwanza, alidai kuwa makontena hayo yaliondolewa bandarini hapo bila kulipiwa kodi na kwamba yeye akiwa meneja hakulijua hilo.

Alidai kuwa awali ulibainika upotevu wa makontena manane, baada ya kufahamishwa na Mrema (ambaye pia alifutiwa mashtaka), lakini baada ya kufuatilia na kisha kuwasilina na TPA, ndipo wakabaini upotevu wa makontena mengine zaidi.

Alidai kuwa hivyo waliamua kuangalia kwenye mfumo wa kompyuta pia hawakuyaona makontena hayo badala yake wakabaini kuwapo kwa makonte zaidi yaliyokuwa hayaonekani na walipowasiliana na TPA, wakaelezwa makontena ambayo hayaonekani ni 54.

Meneja huyo wa AICD aliendelea kudai kuwa baada ya hapo waliendelea kufanya ufuatiliaji kwenye mfumo wao wa kompyuta ndipo wakabaini kuwa jumla ya makontena yaliyokuwa yametoroshwa ni 329.

Alidai kuwa hata majalada ya makontena hayo pia yalikuwa hayaonekani, ndipo yeye kama meneja akatoa amri kwamba hakuna mtu ambaye angeondoka mpaka majalda hayo yapatikane.

Alidai kuwa aliteua timu ya watu wanne wakiongozwa na mshtakiwa Louis, wakaenda kuyafuata mahali ambako yeye hakukujua na kurudi nayo saa sita usiku yakiwa majalada 106 ambayo yana taarifa za makontena hayo 329.

Pia, alibainisha kuwa kuna mtu alimfuata ofisini kwake na kumshawishi kumpa rushwa ili kufunika suala hilo lakini akakataa.

Shahidi mwingine, Hamida Seif, ambaye ni mwandaaji wa taarifa za mizigo AICD, aliieleza mahakama kuwa aliagizwa na mshtakiwa Louis kuondoa taarifa za makontena hayo 329 kwenye mifumo ya taarifa ya TPA na TRA.

“Alianiambia (Louis) kuwa utakapotaka kutuma ripoti, ukikuta ripoti ya Regional Cargo Service Ltd uzitoe,” alidai shahidi huyo akijibu swali la mmoja wa mawakili wa utetezi, Kung’e Wabeya.

Baada ya upande wa mashahidi kufunga ushahidi wake, mahakama hiyo iliwaachia huru washtakiwa wawili, Chimomo na Rupia baada ya kuwaona kuwa hawana kesi ya kujibu huku ikiwataka wengine waliobakia kujitetea baada ya kuwaona wana kesi ya kujibu.

Hukumu ya Mahakama na adhabu

Baada ya utetezi wa washtakiwa hao, Mahakama hiyo katika hukumu yake iliwatia hatiani washtakiwa watatu, Louis, Hassan na Malembo huku ikiwaachia huru Mpande na Omary, baada ya kuridhika kuwa hawana hatia.

Louis na Hassan walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu kila mmoja kwa kila shtaka katika mashtaka 105 ya kughushi na kifungo cha miaka miwili kila mmoja katika shtaka moja la kuisababishia TRA hasara ya Sh12.7 bilioni.

Malembo kwa upande wake alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia katika shtaka moja la kuisababishia TRA hasara ya Sh12.7 bilioni.

Kutokana na mashtaka hayo, Louis na Hassan walihukumiwa adhabu ya kifungo cha jela chenye jumla ya maiaka 317 kila mmoja, lakini akitoa adhabu hiyo Jaji Korosso alisema kuwa adhabu zote zinakwenda pamoja (kwa wakati mmoja) hivyo watatumikia kifungo cha miaka mitatu tu.

Pia, Jaji Korosso aliwaamuru kuilipa TRA fidia nusu hasara ya Sh12,7 bilioni, waliyoisababishia, yaani Sh6.35 bilioni, wote kwa pamoja baada ya kumaliza kifungo chao.

Kwa hukumu hiyo kesi hiyo iliweka rekodi nyingine ya kuwa ya kwanza ya ufisadi kuamuriwa na mahakama hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz