Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utetezi kesi kina Pima wawasilisha pingamizi

Pima Mkurugenzi Jiuji Utetezi kesi kina Pima wawasilisha pingamizi

Thu, 24 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mawakili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dk John Pima na wenzake wawili, wamewasilisha pingamizi mahakamani wakipinga kupokelewa kwa nyaraka tatu.

jana Jumatano Novemba 23, 2022 mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, pingamizi hilo liliwasilishwa na mawakili hao, baada ya shahidi wa 10 wa Jamhuri mfanyabiashara Marita Kivunge(34) kuomba nyaraka hizo zipokelewe kama vielelezo.

Shahidi huyo aliomba nyaraka tano ambazo ni risiti nne kutoka Shirika la Posta Tanzania na dispatch book kutoka kwenye kampuni ya uuzaji wa vifaa na malighafi za ujenzi ya Cherry General Supply and Services. Also Read

Akiwasilisha hoja za pingamizi hilo, wakili wa utetezi Mosses Mahuna aliieleza mahakama kati ya nyaraka hizo wanapinga risiti tatu ambazo zinaonyesha barua zimetumwa kwenda ofisi za katibu Mkuu ofisi ya Rais.

Aliieleza mahakama wakati shahidi huyo anatoa ushahidi wake, aliieleza mahakama kuwa waliandika barua kwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na kutuma nakala ofisi za CAG,PPRA,Takukuru(Arusha),Katibu Tawala mkoa wa Arusha,Katibu Mkuu Tamisemi na Katibu Mkuu Kiongozi.

Alidai kuwa katika risiti hizo alizodai shahidi zimepelekwa kwa ofisi za Katibu Mkuu Tamisemi na Katibu Mkuu Kiongozi,hapo zinasoma Katibu Mkuu ofisi ya Rais huku nyingine ikiwa imeandikwa PPPA.

"Hatuna pingamizi na dispatch book wala risiti iliyoenda kwa CAG,tunapinga hizi tatu ambazo zinakoenda na alichokisema shahidi ni tofauti,"

Naye wakili wa utetezi Sabato Ngogo, aliiomba mahakama isipokee nyaraka hizo kama vielelezo na kuwa zinapingana na ofisi alizotaja shahidi.

Akijibu hoja hizo wakili wa Serikali mwandamizi Timotheo Mmari,aliiomba mahakama kutupilia mbali pingamizi hizo kwani hazina misingi ya kisheria na kuomba nyaraka zipokelewe kama alivyoomba shahidi.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2022 inamkabili Dk Pima,Mariam Mshana(aliyekuwa mwekahazina) na Maduhu.

Awali, akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali mwandamizi Abdallah Chavula,shahidi huyo ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Cherry alidai kuwa Aprili 14,2022 Maduhu alimpigia simu Meneja wa kampuni hiyo Thadei Kessy,akimtaka watoe nyaraka mbalimbali ikiwemo risiti ya kielektroniki ya Sh103 Milioni kabla hawajalipwa fedha hiyo.

Alidai akiwa mkoani Dodoma alipigiwa simu na Kessy akimweleza kuwa amepigiwa simu na Maduhu kuwa kuna malighafi wanazihitaji na kuwa kutokana na kampuni hiyo kudai jiji la Arusha zaidi ya Sh400 Milioni aliwaeleza hawawezi kuwapa malighafi nyingine kwa mkopo.

Hakimu Mkazi Serafini Nsana, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 25,2022 atakapotoa uamuzi mdogo wa pingamizi hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live