Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata wagubika kesi shehena ya dhahabu

43803 Dhahabupic Utata wagubika kesi shehena ya dhahabu

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Utata umeibuka katika kesi ya jinai namba 1/2019 ya kusafirisha shehena ya dhahabu kilo 323.6 na fedha taslimu Sh305 milioni kutoka mkoani Mwanza kuelekea Geita baada ya washtakiwa kutofikishwa mahakamani bila taarifa.

Hadi muda wa Mahakama unamalizika jana Jumatatu washtakiwa 12 wakiwamo askari polisi wanane wanaokabiliwa na shauri hilo hawakufikishwa mahakamani huku Hakimu Mkazi Mwandamizi, Gway Sumaye ambaye shauri linatajwa mbele yake akiiambia Mwananchi hakuwa na taarifa zozote kuhusu washtakiwa hao.

“Nimesubiri sikuona mtu yeyote kuanzia waendesha mashtaka, washtakiwa wala mawakili wa utetezi na sikupata taarifa kwa nini hawajafika; nilichofanya nimeipangia kesi hiyo tarehe nyingine ya kutajwa ambayo ni Machi 13 2019,” alisema Hakimu Sumaye

Washtakiwa wanaokabiliwa na shauri hilo ambalo limeanza kuibua utata kuhusu muda wa kufikishwa mahakamani kubadilika kila mara ni aliyekuwa mkuu wa mperesheni mkoa wa Mwanza mrakibu mwandamizi wa polisi, Morice Okinda, E. 6948 D/CPL. Kasala, F. 1331 PL. Matete, G. 6885 D/C Alex na G. 5080 D/C Maingu.

Wengine waliofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Januari 11 na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na rushwa ni G. 7244 D/C Timothy, G. 1876 D/C Japhet, H. 4060 D/C David Kadama, Hassan Saddiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda ambaye pia anafahamika kwa jina la Paulo Nkinda na Sajid Hassan.

Wakizungumza kwa njia ya simu kwa nyakati tofauti, wakili wa Serikali anayeendesha shauri hilo, Castuce Ndamugoba na mmoja wa mawakili wa utetezi, Antony Nasimile kila mmoja alitoa maelezo tofauti kuhusiana na washtakiwa kutofikishwa mahakamani kama ilivyokuwa kwenye kalenda ya Mahakama.

Wakati Wakili Ndamugoba akisema naye alikuwa mahakamani kusubiri washtakiwa kutoka mahabusu ya Gereza Kuu la Butimba wanakohifadhiwa, wakili Nasimile alisema alipewa taarifa kuwa wateja wake wasingefikishwa mahakamani hadi Machi 11.

Alipoelezwa upande wa utetezi umepewa taarifa ya wateja wao kutofikishwa mahakamani, wakili wa Serikali alisisitiza kutokuwa na taarifa hizo na kuelekeza atafutwe mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa (RCO) Mwanza, Faustine Mafwere kwa maelezo zaidi.

“Sisi tulikuwa hapo mahakamani na bado tunawasubiri (washtakiwa). Hatujafahamu kwa nini hawakuletwa, pengine mpigie simu RCO anaweza kukwambia sababu ni nini,” alisema Ndamugoba.

Muda wa washtakiwa hao kufikishwa mahakamani umekuwa ukibadilika ambapo badala ya kupelekwa mahakamani na gari linalobeba washtaki wengine wao hutumia magari maalum huku wakifikishwa nyakati za mchana badala ya asubuhi kama ilivyo kwa washtakiwa walioko mahabusu.

Ingawa haijawekwa wazi, kuna madai mabadiliko ya muda na ratiba ya kuwafikisha mahakamani washtakiwa hao inalenga kuwakwepa waandishi wa habari wanaofuatilia kesi hiyo kwa karibu.

Juhudi za kumpata kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.



Chanzo: mwananchi.co.tz