Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utata bastola mbele ya RC, RPC

36717 Pic+bastola Utata bastola mbele ya RC, RPC

Wed, 16 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Jeshi la Polisi linachunguza tukio la mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Emanuel Kisoka kudaiwa kumtolea bastola mfanyabiashara wa Moshi, Baraka Olotu.

Tukio hilo linadaiwa kutokea mita chache kutoka alipokuwa ameketi mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira na kamanda wa Polisi mkoani humo, Hamis Issah.

Kamanda Issah alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alikiri kuwepo na kuahidi kulitolea taarifa leo, ingawa alisema kwa sasa wanachunguza uhalali wa umiliki wa silaha hiyo.

“Ngoja nilifuatilie nijue limefikia wapi na kosa la msingi ni lipi kwani bado anashikiliwa na ilikuwa atolewe akalete kadi yake kwa kuwa kumiliki silaha siyo kosa ila kusababisha fujo ni kosa,” alisema Issah.

Taarifa zilizopatikana jana zilidai tukio hilo lilitokea Desemba 26, 2018 usiku katika kilabu maarufu ya Redstone ya mjini Moshi ambayo siku hiyo ilikuwa imejaa wateja wakiwamo raia wa kigeni.

Akizungumza na gazeti hili jana, Olotu alidai siku hiyo akiwa katika kilabu hiyo kulitokea kutoelewana na Kisoka maarufu kwa jina la Chidi, na ndipo alipochomoa bastola hiyo.

“Pale kwenye baa ya Garden (ya wazi) alikuwepo pia RC (mkuu wa mkoa) na RPC (kamanda wa polisi mkoa) na (Chidi) alikamatwa na kupelekwa polisi, lakini mpaka sasa hajafunguliwa mashtaka,” alisema Olotu.

Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, baada ya tukio hilo alifungua jalada polisi lenye namba MOS/RB/11660/18 na kwamba wakati wa purukushani za kumkamata mfanyabiashara huyo RC na RPC waliona.

Hata hivyo, Kisoka alipotafutwa na Mwananchi jana alikiri kutokea kwa purukushani, lakini akakanusha kuchomoa bastola akidai walinzi ndio waliohamaki baada ya kuiona.

“Hii issue (suala) ikitokea hata RPC alikuwepo. Mimi nilikuwa naamua tu ugomvi kati ya Olutu na vijana fulani ndio wale ma-bouncer (walinzi) wakaiona ndio waka-panic (wakahamaki),” alisema.

“Tulikwenda hadi kituo cha kati (cha polisi) na baada ya kujieleza wakaona hakuna jinai imetendeka wakanitaka nilete vibali, kesho yake nikapeleka nikarudishiwa bastola yangu.”



Chanzo: mwananchi.co.tz