Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utaratibu rufaa wananchi Ngorongoro wawekwa

Hukumu Pc Data Utaratibu rufaa wananchi Ngorongoro wawekwa

Tue, 7 Feb 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki imeweka utaratibu wa kusikiliza rufaa iliyofunguliwa na halmashauri za vijiji vinne vilivyopo wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania.

Rufaa hiyo namba 13/2022 inapinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), mwaka jana iliyotupilia mbali maombi ya wananchi kutoka vijiji hivyo, walioishitaki serikali ya Tanzania wakidai kuondolewa kwenye maeneo yao kwa nguvu nje ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Jana Jumatatu Februari 6, 2023,Mahakama hiyo ilipanga kutaka rufaa hiyo kwa ajili ya kupanga utaratibu wa kuisikiliza mbele ya jopo la Majaji watano wakiongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Nestor Kayobera, Jaji Sauda Mjasiri, Jaji Anita Mugeni, Jaji Kathurima M'Inoti na Jaji Cheborion Barishaki.

Kwa upande wa mjibu rufaa aliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Vivian Method na wakili wa serikali, Narindwa Sekimanga huku waleta rufaa wakiwakilishwa na mawakili watano wakiongozwa na Rais wa Chama cha wanasheria Afrika (PALU) Donald Deya, Esther Muigai, Jebra Kambole, Praisegod Josep na Joseph Oleshangay.

Baada ya majadiliano baina ya pande zote mbili waleta maombi na wajibu maombi waliomba muda wa mwezi mmoja kuwasilisha hoja zao kwa njia ya maandishi pamoja na muda wa siku 14 kuwasilisha hoja za nyongeza.

Akisoma utaratibu huo Jaji Kayobera, amesema waleta rufaa watawasilisha hoja zao kwa njia ya maandishi Machi 6, upande wa wajibu rufaa kujibu Aprili 5, 2023 kisha pande zote kuwasilisha hoja za nyongeza Aprili 19, mwaka huu kabla ya mahakama kupanga katika kikao chake cha Mei.

Katika siku hiyo amesema pande zote mbili zitawasilisha kwa mdomo kwa muda wa nusu saa, kisha kupanga tarehe ya uamuzi.

Awali Septemba 30, 2022 mahakama ya EACJ ilitoa hukumu katika kesi namba 27/2017 ambapo ilitupilia mbali shauri hilo.

Jaji Justice Nyachaye amesema waombaji hao wafugaji wa jamii ya kimasai walishindwa kuthibitisha madai ya kuteswa na kupigwa na kuwa hawakuweza kutoa ushahidi kwamba mali zao ziliharibiwa na watu waliowataja kuwa askari wa jeshi la polisi.

Shauri hilo lililofunguliwa mahakamani hapo Septemba 12, 2017 na vijiji vya Olososokwani, Olorien, Kirtalo na Arashi waliodai vijiji vyao vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria.

Chanzo: mwanachidigital