Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushauri wa Kinana kwa IGP wazua gumzo

Ushauri Pic Data Ushauri wa Kinana kwa IGP wazua gumzo

Mon, 1 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni kama amewawashia moto, hivi ndivyo unavyoweza kuuelezea ushauri wa Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulrahman Kinana, alimpomshauri Inspekta Jenerali wa Polisi, Camilius Wambura kupunguza idadi ya trafiki barabarani.

Ushauri huo umepokewa kwa hisia tofauti na wananchi, wasafirishaji na wadau wa usalama, wengine wakiunga mkono na wengine wakipinga kuwa kama hilo litafanyika, nchi inaweza kutumbukia katika wimbi la ajali za kutisha.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Kinana, aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki na Katibu mkuu wa CCM, ambayo imekuja baada ya Rais Samia Suluhu naye kuwahi kuwanyooshea kidole, imeungwa mkono na madereva karibu mikoa yote.

Madereva wengi waliopaza sauti zao, wanadai trafiki wengi wamekuwa kero barabarani kwa kusimamisha magari kila baada ya kilomita chache, huku wengine wakidaiwa kuwabambikia madereva makosa ili kutengeneza mazingira ya rushwa.

Hata hivyo, baadhi ya madereva, wananchi na mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), wanasema kama uwepo wa trafiki unaonekana ni mkubwa, huku makosa ya barabarani yakiwa mengi, basi jamii itegemee ajali za kutisha ikiwa trafiki watapunguzwa.

“Kama trafiki ni wengi na madereva wana overtake vibaya na kwenda spidi za hatari ndio wakipunguzwa itakuwaje? Kama kuna trafiki ni kero washughulikiwe wao tusiwachanganye kapu moja,” alidai Charles Mboya, mkazi wa Moshi.

Mkurugenzi wa RSA Tanzania, Fungo Augustus alisema kwa uzoefu wake trafiki hawatoshi nchi nzima, akisema hoja inaweza kuwa hao trafiki wachache wanagawanywaje na wakishapangiwa kazi, wanafanya kazi waliyopangiwa? Mwenyekiti wa RSA Mkoa wa Kilimanjaro, Khalid Shekoloa alienda mbali na kueleza kupunguzwa kwa trafiki barabarani wakati waliopo hawatoshi, ni sawa na kukaribisha utawala wa manyani.

IGP apokea ushauri

Kutokana na uzito wa kauli hiyo, IGP Wambura alilieleza gazeti hili akisema: “Ushauri uliotolewa ni mzuri na ninaupokea na nakwenda kuufanyia kazi kwenye taasisi yangu.” Awali, Jeshi la Polisi kupitia kwa msemaji wake, David Misime, lilijitokeza na kutoa taarifa kwa umma likisema limeanza kuufanyia kazi ushauri wa Kinana na kuweka mikakati mizuri.

Kauli ya Kinana si ya kwanza, kwani Desemba 21, 2021, Rais Samia aliwataka trafiki nchini kuwa na lugha nzuri kwa raia.

Imeandikwa na Daniel Mjema Mussa Juma, Furtune Francis, Peter Saramba, Mgongo Kaitira Rehema Matowo, Ramadhan Hassan, Hawa Mathias na Lilian Lucas.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live