Ushahidi bora wa Marwa Mariba (5) aliyekuwa shahidi wa Pili wa Jamhuri umeishawishi Mahakama kumuona baba mdogo wake aitwaye Baru Nyaigera, ana hatia ya mauaji ya baba wa mtoto huyo hivyo kumhukumu kunyongwa hadi kufa.
Mtoto huyo ndiye shahidi pekee wa Jamhuri aliyeshuhudia mauaji ya Mariba Nyaigera yaliyotokea saa 2:00 asubuhi ya Januari 17, 2023 katika kijiji cha Kimusi katika wilaya ya Tarime, ambapo Baru alimuua kaka yake kwa kumkata na panga shingoni.
Ushahidi wake huo ulikuwa ni mzito kiasi kwamba hata alipododoswa maswali na wakili wa mshitakiwa, bado alikuwa imara na hakutetereka huku akisisitiza kushuhudia mauaji ya baba yake na ndipo alipokimbia kwenda kumuita bibi yake.
Hukumu hiyo ilitolewa jana Jumatatu, Machi 25, 2024 na Jaji Marlin Komba wa Mahakama Kuu kanda ya Musoma iliyopo Tarime, ambaye alisema kosa la mauaji ya kukusudia linapothibitishwa, adhabu ni moja tu nayo ni kunyongwa hadi kufa.
Katika kuthibitisha shitaka hilo, upande wa mashitaka uliita mashahidi wanne ambao ni Mgusi Nyaigera aliyekuwa shahidi wa kwanza, Marwa aliyekuwa shahidi wa pili, Dk Christopher Chacha aliyekuwa shahidi wa tatu na Sajini Godfrey, shahidi wa nne.
Ushahidi wa mtoto ulivyokuwa
Akitoa ushahidi wake, Mara aliyekuwa na umri wa miaka mitano, aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio alikuwa na baba yake shambani na kusema kwa sasa anajua yuko kaburini na sababu ya kuwa kaburini ni kwa sababu amekufa.
Hata kabla ya kuongozwa na wakili wa Jamhuri kutoa ushahidi, mtoto huyo alimnyooshea kidole mshitakiwa aliyekuwa kizimbani kwamba ndiye aliyemuua baba yake ambaye kwa wakati huo akitoa ushahidi yuko kaburini.
Alipoulizwa namna mshitakiwa alivyomuua baba yake, alieleza kwamba alimkata baba yake kwa panga kwenye shingo na kumtaja mtu aliyemuua kwa jina la ‘Baba Baru’ ambaye ni baba yake mdogo anayezaliwa tumbo moja na baba yake.
Wakati akiendelea kuelezea nini kilitokea, aliieleza mahakama kuwa siku hiyo yeye alikuwa shambani na baba yake na mshitakiwa alikuwa pia kwenye shamba lake tofauti na la baba yake na ndipo alipomuona mshitakiwa akimkata baba yake.
Kulingana na uchambuzi wa ushahidi huo uliofanywa na Jaji, baada ya kuona Baru amemkata baba yake shingoni kwa panga, alikimbia na kwenda kumuita bibi yake, Mgusi Nyaigera ambaye naye alimuita mtu mwingine na kukimbilia eneo la tukio.
Akidodoswa zaidi na wakili wa mshitakiwa, mtoto huyo alieleza kuwa mshitakiwa ndiye alimkuta kaka yake shambani akipanda mtama na kwamba panga lililotumika kumkata Mariba halikuwa la marehemu bali lilikuwa ni la mshitakiwa.
Katika ushahidi wake, shahidi wa pili, Mgusi Nyaigera ambaye ni mama wa marehemu, alieleza kuwa siku ya tukio alikuwa nyumbani kwake akifagia, ghafla akamuona anakuja akilia na kumweleza kuwa baba yake amekatwa na panga.
Kwa vile shamba lilijuwa jirani na nyumba yake, alitazama na kumuona marehemu akija usawa wa kuelekea nyumbani mwili wake wote ukiwa umelowa damu na hakuweza kufika mbali kwani alianguka njiani kabla ya kufika nyumbani.
Hapo alimuona mshitakiwa ambaye ni mtoto wake akiwa hatua chache kutoka shambani ameshika panga lililokuwa na madoadoa ya damu ambapo alipiga yowe kuomba msaada kutoka kwa majirani, na baadhi walijitokeza kutoa msaada.
Hata hivyo, majirani hao walipomuona mshitakiwa ameshika panga, wote walikimbia na baada muda kupita, majirani walianza kujikusanya tena na muda mfupi baada aliona askari polisi wamefika wakiwa wameongozana na daktari.
Katika ushahidi wake, Dk Ugungo alipofika alithibitisha kuwa Mariba tayari ni marehemu na katika uchunguzi wa mwili wa marehemu, alibaini sababu za kifo ni kukatwa mshipa mkuu wa damu unaosambaza damu kwenda kwenye moyo.
Kwa upande wake, mpelelezi wa kesi hiyo, Askari mwenye namba G.6047 Sajini Godfrey kutoka kituo cha polisi Nyamwaga alisema alipofika eneo la tukio alikuta tayari mshitakiwa amekamatwa na eneo la tukio kulikuwa na dimbwi la damu.
Katika utetezi wake, alijitetea kuwa siku ya tukio analohusishwa nalo, alikuwa nyumbani kwake lakini akaamua kwenda shambani na ndipo alipomkuta kaka yake akiwa amesogeza majani ambayo yanatenganisha mpaka wa shamba lake.
Alieleza kuwa aliamua kurudisha mpaka kwenye eneo lake na ndipo kaka yake alimpiga kwa jembe kwenye mbavu na yeye akakimbia na kuchukua panga lililokuwa umbali wa kama hatua tano kutoka mahali walipokuwa wawili hao.
Wakati huo mshitakiwa alikuwa na panga na marehemu alikuwa na jembe na akajitetea kuwa marehemu alijigonga mwenyewe kwenye panga aliloshika na baada ya hapo alienda kwa mjomba wake, Mwita Wayangi na ndipo alipokamatiwa.
Hukumu ya Jaji Komba
Jaji Komba katika hukumu yake alisema baada ya kukamilika kwa usikilizwaji wa ushahidi wa pande mbili, ni jukumu la mahakama ni kuamua kama ni kweli mshitakiwa aliyepo kizimbani ndiye aliyesababisha kifo cha marehemu Mariba.
“Hakuna ubishi kuwa Mariba amekufa na kifo chake si cha kawaida kwa kuwa alikuwa na jeraha la kukatwa na kitu chenye ncha kali katika shingo kilichokata mshiba mkubwa wa damu na kutokwa na damu nyingi,”alisema Jaji Komba.
Jaji alisema shahidi wa pili ambaye ni mtoto wa marehemu na ambaye alishuhudia mauaji hayo yaliyotokea saa 2:00 asubuhi ameeleza namna alivyoshuhudia mshitakiwa aliyeko kizimbani akimkata marehemu kwa panga.
Baada ya kushuhudia mauaji hayo, mara moja alikimbilia kwa bibi yake ambaye alimkuta mshitakiwa akiwa na panga shambani na kwa wakati huo kulikuwa na watu wawili tu shambani, yaani mshitakiwa Baru na marehemu Mariba.
Jaji alisema baada ya mama yao huyo kumuona marehemu akiwa amelowa damu na mshitakiwa akiwa ameshika panga, alipiga yowe na mshitakiwa akakimbia kutoka eneo la tukio baada ya yowe hilo la mama yake mzazi.
“Ilikuwa ni mchana kweupe hivyo uoni wa mashahidi wote wawili haukuwa umeathiriwa na kitu chochote. Shahidi wa 2 anamfahamu mshitakiwa kama baba yake mdogo na anamfahamu marehemu kama baba yake mzazi,”alisema Jaji.
Katika kuamua kama utambuzi wa shahdi wa pili (mtoto) ulikuwa mzito, ni lazima ushahidi wake lazima upimwe kuhakikisha utambuzi huo ulikuwa sahihi ili mahakama iweze kuuamini na katika kesi hii, tukio lilitokea asubuhi saa 2:00.
“Ni ukweli kuwa huko shambani walikuwepo watu watatu tu na shahidi wa kwanza (Mgusi) aliposogelea shambani alimuona mshitakiwa akiwa ameshika panga lililokuwa na madoa doa ya damu,” alieleza Jaji Komba katika hukumu.
“Kwa uchambuzi wa mahakama ninaona mshitakiwa alitambuliwa kikamilifu na shahidi wa kwanza na wa pili. Ushahidi wao umeziba uwepo wa mazingra kuwa labda alitambuliwa kimakosa (mistaken identity),”alisema Jaji huyo na kuongeza:-
“Shahidi wa pili aliieleza mahakama kuwa Baru alitumia panga kumkata shingo baba yake. Mshitakiwa amekuwa mahabusu tangu alipokamatwa lakini shahidi alipopanda kizimbani amemkumbuka ndiye alimkata baba yake kwa panga na kumuua”
“Sina sababu ya kutoamini ushahidi wa aina hiyo. Ili kosa la mauaji lithibitishwe kuna vigezo vinne. Moja lazima kuwe na kifo, pili kiwe kimesababishwa na tendo lisilo halali kisheria, tatu, mshitakiwa ndio alifanya na nne kuwe na nia ovu”
Katika kesi hii, Jaji alisema kuna mtu anaitwa Mariba Nyaigera ambaye alikuwa na kifo chake ni cha mashaka kwa kuwa na jeraha la kukatwa shingoni ambalo lilisababisha kuvuja damu nyingi na kufariki na mshitakiwa kuhusisha na kifo.
Jaji alisema katika kesi hiyo, mshitakiwa alitumia panga kumkata marehemu, pigo ambalo lilielekezwa kwenye shingo na kuathiri mishipa ya damu na ripoti ya daktari inaonyesha ilikata mishipa iliyofanya marehemu kutokwa na damu nyingi.
“Panga ni silaha hatari sana na eneo lililoshambuliwa ni shingo ambayo ni nyeti (sensitive) la mwili wa mwanadamu. Pigo moja lilikuwa kubwa kwa kuwa marehemu alikufa dakika chache tu baada ya kupigwa pigo hilo,”alisema Jaji.
“Jeraha lilikuwa baya na liliingia ndani kwenye shingo na mshitakiwa alitoroka eneo la tukio. Hii inaonyesha kwamba alidhamiria kumuua marehemu kwa kuwa vigezo vyote vya kuthibitisha uwepo wa nia ovu (malice) vimethibitishwa”
Jaji alisema kwa kupima ushahidi wote kwa ujumla wake, anaona upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha shitaka hilo bila kuacha shaka, hivyo anamtia hatiani na kwa kuwa adhabu ya kosa hilo ni moja, anamhukumu adhabu ya kifo.