Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushahidi wa marehemu kutumika kesi ya Kitilya

41487 Pic+kitilya Ushahidi wa marehemu kutumika kesi ya Kitilya

Thu, 14 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Maelezo ya Ramadhan Khijja aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Fedha katika Serikali ya Awamu ya Nne, ni miongoni mwa ushahidi utakaotumika katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wenzake wanne.

Jumla ya mashahidi 54 wanatarajia kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Miongoni mwao ni pamoja na aliyewahi kuwa waziri wa Fedha Mustafa Mkulo, mwanasheria mkuu wa Serikali wa zamani Jaji Frederick Werema, mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey Mgimwa na mashahidi wengine saba kutoka Uingereza.

Hata hivyo, Khijja alishafariki dunia, lakini maelezo yake yatatumika kama ushahidi katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Jopo la mawakili watano wa Serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Fredrick Manyanda akisaidiana na Tumaini Kwema, George Barasa, Ester Martin na Leonard Swai kutoka Takukuru jana liliwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili Manyanda aliwataja mashahidi hao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati akiwasomea washtakiwa hao maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Mbali na mashahidi hao, pia vielelezo 218 zikiwemo nyaraka na barua mbalimbali vitatolewa mahakamani hapo.

Wakili Kweka alitaja baadhi ya nyaraka zilizopo katika vielelezo hivyo kuwa ni maelezo ya onyo ya washtakiwa wote, barua za mawasiliano baina ya washtakiwa na benki, barua za kufungulia akaunti za benki na nyaraka za kufungua kampuni kutoka Brela.

Nyaraka nyingine ni mawasiliano ya barua pepe baina ya washtakiwa, nyaraka kutoka nje ya nchi pamoja na hundi mbalimbali.

Hatua hiyo ya kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo washtakiwa hao, imehitimisha na kufungwa rasmi kwa kesi hiyo katika Mahakama ya Kisutu.

Jalada la kesi hiyo sasa limehamishiwa rasmi Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, na litapangiwa tareha kwa ajili ya kuanza kutoa ushahidi.

Baada ya upande wa mashtaka kumaliza kuwasomea maelezo na vielelezo vilivyochukua saa mbili na nusu, Hakimu Shahidi alisema mahakama ya Kisutu imetoa amri ya kuhamishia shauri hilo katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

“Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa amri ya kuhamishia shauri hili Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,” alisema Hakimu Shaidi.

Mashtaka yao

Kitilya na wenzake wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 58, mashtaka 49 kati ya hayo ni ya utakatishaji fedha, matatu ya kughushi na mawili ya kutoa nyaraka za uwongo.

Mashtaka mengine yanayowakabili ni kuongoza mtandao wa uhalifu uliosababisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata hasara ya dola za Marekani 600milioni, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kula njama za kutenda kosa kwa nia ya kumdanganya katibu mkuu Wizara ya Fedha.

Mbali na Kitilya, washtakiwa wengine ni Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon ambao walikuwa maofisa wa Stanbic Bank.

Wengine ni aliyekuwa kamishna wa sera na madeni Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda (kwa sasa yuko Ofisi ya Waziri Mkuu) na Alfred Misana, ambaye alikuwa kamishna msaidizi wa serana madeni kutoka wizara hiyo ambaye kwa sasa yuko wizara ya afya.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na nje ya nchi.

Makosa hayo yalitokana na mchakato kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekeni 550milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingereza kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4, kupitia kampuni ya Egma T Ltd. Katika mashtaka hayo wanadaiwa kujipatia Dola za Marekani 6milioni kwa njia za udanganyifu kupitia kampuni ya Enterprises Growth Market Advisors (Egma) kama ada ya uwezeshaji wa mkopo huo ya asilimia 2.4 na kisha kutakatisha kiasi hicho cha fedha.

Chanzo: mwananchi.co.tz