Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushahidi wa kupikwa ‘wamchomoa’ gerezani aliyefungwa kwa kubaka

Kubaka?fit=759%2C398 Ushahidi wa kupikiwa

Fri, 20 Aug 2021 Chanzo: IPPmedia

Mkazi wa Mafinga mkoani Iringa, Onesmo Makoga, ametolewa gerezani alikokuwa amefungwa maisha baada ya Mahakama Kuu kubaini ushahidi wa kubaka uliomtia hatiani ulikuwa umepikwa. Hukumu hiyo ilitolewa Agosti 19, katika Mahakama Kuu Kanda ya Iringa mbele ya Jaji Joseph Mlyambina baada Makoga kukata rufani.

Mlalamikaji alishtakiwa kwa kubaka katika Mahakama ya Wilaya ya Mufindi kwa madai kwamba alitenda kosa hilo Agosti 26, 2017.

Mlalamikaji huyo anadaiwa kubaka mtoto wa darasa la kwanza na katika usikilizaji wa shauri hilo, alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Katika sababu za rufani, Makoga alidai kuwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya alikosea kumtia hatiani na kumpa adhabu hiyo kwa kuangalia ushahidi wa Jamhuri ambao ulishindwa kuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka.

Pia alidai kuwa mahakama ilikosea kudharau utetezi wa mlalamikaji na kwamba ushahidi wa shahidi wa kwanza ambaye ni mtoto, ulikuwa wa kupandikizwa na kwamba tukio linadaiwa kutokea Agosti 26, 2017 wakati siku hiyo ilikuwa Jumamosi na watoto hawaendi shuleni na yeye alikuwa shambani.

Wakili wa Jamhuri, Alice Thomas, akijibu hoja, alidai mtoto alikuwa anakwenda katika masomo ya ziada na wakati wa usikilizwaji hakukuwa na swali kuhusu siku hiyo, hivyo hoja hiyo ya mlalamikaji ameiibua katika rufani.

Katika uamuzi wa rufani hiyo, Jaji Mlyambina alisema upande wa Jamhuri haukueleza mtoto huyo alikuwa darasa la kwanza na alitakiwa kuhudhuria masomo ya ziada.

"Nakubaliana na wakili wa upande wa Jamhuri kwamba hakukuwa na maswali kuhusiana na siku ya tukio kwamba ilikuwa Jumamosi lakini upande wa Jamhuri ulikuwa na jukumu la kufafanua kwa nini mtoto alienda katika masomo ya ziada siku ya Jumamosi.

"Siku hiyo kwa mazingira ya kawaida, wanafunzi hawaendi shuleni labda wanafunzi wanaotakiwa kufanya mtihani wa taifa kwa mwaka huo. Nakubaliana na mlalamikaji kwamba hii ni moja ya kesi ambazo ushahidi wake umepikwa. Ushahidi wa mtoto haukuwa mzuri," alisema Jaji Mlyambina.

Mlalamikaji alidai shahidi wa pili ambaye ni mama wa mtoto, alimlazimisha mwanawe kwa kumpiga ili aseme kabakwa.

Hoja hiyo ilipingwa na Wakili wa Jamhuri, ambaye alidai mlalamikaji alimfunga mdomo mtoto ili asiseme ukweli kitendo kilichomfanya mama atumie nguvu ili aseme ukweli.

Jaji Mlyambina alisema katika tukio hilo kuna mkanganyiko katika ushahidi wa shahidi wa kwanza ambaye ni mtoto na shahidi wa pili ambaye ni mama.

Katika ushahidi mtoto anadai alitolewa nje ya nyumba na mama yake akawa anamhoji wakati mama anasema alichukua fimbo akamchapa ili aseme alichofanyiwa.

"Ushahidi kama huu unaonyesha umepikwa. Ushahidi wa shahidi wa kwanza na shahidi wa pili hauonyeshi kama aliyebaka ni mlalamikaji.

“Nimeona mlalamikaji alitoa sababu dhaifu wakati anapinga kupokelewa kwa kielelezo cha maelezo yake, ushahidi wa shahidi wa nne hauungani na ushahidi wa mashahidi wengine.

"Nakubaliana na mlalamikaji kwamba Hakimu alidharau ushahidi wake wa utetezi akakubali ushahidi wa upande wa Jamhuri ukiwamo wa mtoto ambao umepikwa.

"Upande wa Jamhuri haikuthibitisha mashtaka bila kuacha shaka, kutiwa hatiani na adhabu ya kifungo cha maisha aliyopewa mlalamikaji inafutwa, aachiwe huru," alisema Jaji Mlyambina.

Chanzo: IPPmedia