Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushahidi kuendelea kesi ya Sabaya

9092c2ec1445e9d727b869f828e0f542 Ushahidi kuendelea kesi ya Sabaya

Mon, 7 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa nne katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita leo anatarajiwa kuanza kujitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha.

Awali shahidi wa tatu wa utetezi, Sabaya aliongozwa na mawakili wake Mosses Mahuna na Faudhia Mustapher na baadae alihojiwa na waendesha mashitaka waandamizi wa serikali ambao walimaliza kumhoji wiki iliyopita.

Mawakili hao walimhoji shahidi huyo kwa siku tatu mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda na baadaye aliendelea kuongozwa tena na mawakili wake.

Sabaya leo anaweza kumaliza kutoa ushahidi wa kujitetea ili kutoa fursa kwa shahidi wa nne apande kizimbani kutoa ushajidi.

Wakati Sabaya akihojiwa na waendesha mashitaka wa serikali ilidaiwa kuwa nyaraka za kampuni ya simu ya Vodacom ambacho ni kielelezo cha tatu (P3) zilionesha simu namba 0758 70 71 71 iliyosajiliwa kwa jina la Sabaya ikionesha kwamba kati ya Januari 22 mwaka jana hadi Januari 25 mwaka huo iliwasiliana mara 27 na mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, Enock Mnkeni (41) katika maeneo ya jijini Arusha.

Mbali ya Sabaya washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Enock Mnkeni (41), Watson Mwahomange (27), John Aweyo (45), Syliverster Nyegu (26) ambaye ni Msaidizi wa Sabaya, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Katika shitaka la kwanza ilidaiwa kuwa Januari 20 mwaka jana ndani ya Jiji la Arusha Sabaya alitumia vibaya madaraka yake na kuongoza genge la uhalifu.

Katika shitaka la pili, Sabaya anadaiwa kuwa Januari 20 mwaka jana ndani ya Jiji la Arusha na alishiriki kuomba rushwa ya shilingi milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara, Francis Mrosso.

Katika shitaka la tatu Sabaya anadaiwa kuomba rushwa ya shilingi milioni 90 kwa Mrosso ili aweze kumsaidia katika kesi ya jinai ya ukwepaji kodi iliyokuwa ikimkabili.

Katika shitaka la nne anadaiwa kuwa Januari 20 mwaka jana ndani ya Jiji la Arusha aliomba rushwa ya shilingi milioni 90 kutoka kwa Mrosso.

Katika shitaka la tano la utakatishaji fedha haramu linalowakabili washitakiwa wote wanadaiwa kuwa Januari 20 mwaka jana, ndani ya Jiji la Arusha walichukua fedha shilingi milioni 90 kwa Mrosso na kwenda kuzifanyia matumizi yasiyokuwa halali kinyume na sheria ya utakatishaji fedha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live