Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushahidi kesi ya Zumaridi wafungwa

Zumaridiipic Data Ushahidi kesi ya Zumaridi wafungwa

Wed, 23 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ushahidi wa Jamhuri katika kesi namba 12 ya kufanya mkusanyiko usio halali  inayomkabili Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi na wafuasi wake 83 umefungwa leo katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza.

Kufungwa kwa ushahidi huo kumekuja baada ya upande wa Jamhuri ulioongozwa na mwendesha mashtaka mwandamizi Dorcas Akyoo kudai mahakamani hapo kuwa hawataleta shahidi mwingine katika kesi hiyo.

Shahidi wa mwisho katika kesi hiyo alikuwa ni Askari mwenye namba F,1368 Sajenti Robert ambaye awali maelezo aliyomwandika mshitakiwa namba moja Diana Bundala marufu kama mfalme Zumaridi  yalipingwa na mawakili wa utetezi na kusababisha kuibuka kesi ndogo ndani ya kesi ya kubwa.

Katika kesi hiyo Upande wa Jamhuri umeleta jumla ya mashahidi tisa na vielelezo vinne yakiwemo maelezo ya mshitakiwa namba moja Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi yaliyopokelewa mahakamani hapo wiki iliyopita na kuombwa na upande wa Jamhuri  yatumike kama kielelezo.

Akitoa ushahidi wake Robart ameiambia mahakama kuwa Februari 22 mwaka huu majira ya mchana  alimuonya Zumaridi kwa kosa la kufanya mkusanyiko usio halali baada ya kumsomea haki zake ambapo mshitakiwa alimuomba askari huyo achukue maelezo yake kwani  hana uwezo wa kuandika kwa haraka mwenyewe

Jopo la mawakili wa utetezi ukiongozwa na  Erick Mutta ulidai  kuwa wakati shahidi wa Jamhuri Robert akitoa ushahidi wake hakuieleza mahakama kuwa kabla kumuonya  alipata maelekezo yoyote kutoka kwa mkubwa wake kuwa atamhoji kwa jambo gani.

Aidha wakili Mutta alidai kuwa pamoja na shahidi huyo  kuieleza mahakama kuwa mshitakiwa namba moja wakati akichukuliwa maelezo yako alikiri kutenda kosa lakini katika maelezo aliyomwandika hakuna popote  panapoonyesha alikari kutenda kosa gani.

Baada ya kusikiliza pande zote Hakimu Mkazi Clescensia Mushi anayesikiliza kesi hiyo akaiahirisha hadi Desemba 6 mwaka huu atakapotoa maamuzi madogo kama Zumaridi na wafuasi wake wana kesi ya kujibu au la.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live