Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upungufu hati ya mashtaka wakwamisha kesi ya kubaka

46314 PIC+HATI Upungufu hati ya mashtaka wakwamisha kesi ya kubaka

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi ya kubaka inayomkabili Mkazi wa Stakishali, Leonard Sule (41) imeshindwa kuanza kusikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya Wakili wa Serikali, Grace Lwila kubaini mapungufu katika hati ya mashtaka.

Wakili Lwila amesema hayo leo Jumanne Machi 12, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Catherine Kihoja akisisitiza kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Ameeleza kuwa wakati akimuandaa shahidi ili aanzE kutoa ushahidi wake mahakamani hapo, alibaini kuwa hati ya mashtaka ina upungufu na hivyo ameomba mahakama impatie nafasi ili kufanya marekebisho ya upungufu huo. Hakimu Kihoja alikubaliana naye na kuiahirisha kesi hadi Aprili 5, 2019.

Siku hiyo kesi itatajwa na iwapo upande wa mashtaka utakuwa umekwishafanya marekebisho hayo mshtakiwa atasomewa hati ya mashtaka na maelezo ya awali (PH). Upelelezi wa kesi hiyo ulikwisha kamilika na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 639 ya mwaka 2018, katika eneo la Pugu, Sule anadaiwa kati ya Oktoba Mosi na 10, 2018 alimbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 16.

Mshtakiwa andaiwa kufanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 130(1)(2)(e) na 131(1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002. Alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 6, 2018.



Chanzo: mwananchi.co.tz