Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi wa washtakiwa wa 'nitumie hela kwenye namba hii' haujakamilika

Sat, 22 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Upelelezi katika kesi ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno (sms) kwa watu tofauti tofauti maarufu kama 'nitumie hela kwenye namba hii' inayowakabili washtakiwa 13, bado haujakamilika.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matano, likiwemo la utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh154 milioni, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi, ameieleza mahakama hiyo leo Septemba 21, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hili bado haujakamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upelelezi umekamilika" alidai Kishenyi.

Wakili Kishenyi baada ya kueleza hayo, Hakimu Mhina aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 2, kesi hiyo itakapotajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni Boniface Maombe, David Luvanda, Moshi Sungura, Amos Bosco, Lule Kadenge, Jofrey Kapangamwaka, William Nturo, Regius Mauka, Collins Mwang'omolan, Francis Kapalata, Kasonde Kapela, Enock Mwandaji na Pascal Kiatu.

Kwa pamoja  wanadaiwa kutenda makosa hayo, kati ya Machi 6 na Juni 2018 jijini Dar es Salaam, Rukwa na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kipindi hicho, washtakiwa walikula njama kwa kutuma ‘sms’ zisizotakiwa katika maeneo ya Dar es Salaam, Rukwa na sehemu zingine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo zikiwa katika muundo wa jumbe fupi (SMS), kupitia mfumo wa kompyuta kwa nia ya kudanganya.

Pia, wanadaiwa kusambaza meseji za kielektroniki zisizotakiwa kupitia mfumo wa kompyuta.

Katika shtaka la nne , katika kipindi hicho kwa njia ya kudanganya na kushawishi, walisambaza jumbe fupi za kielektroniki kwenda kwa watu tofauti tofauti wakionyesha kuwa wanayo mamlaka ya kufanya hivyo wakati si kweli.

Shtaka la tano wanadaiwa kati ya Machi na Juni 2018 mkoani Rukwa na katika maeneo ya Dar es Salaam na sehemu nyingine za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania washtakiwa kwa pamoja walijihusisha na muamala wa Sh 154,032, 830 huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo wala kutoa dhamana hadi Mahakama Kuu kwa kuwa shtaka la utakatishaji fedha ni miongoni kwa mashtaka yasiyo na dhamana.

Chanzo: mwananchi.co.tz