Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi wa tukio la Hamza kuvuka mipaka

Gaidi Mtuhimiwa wa ugaidi, Hamza kabla ya kuuawa na polisi

Wed, 8 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema upelelezi dhidi ya tukio la Hamza Mohammed, ni endelevu kwa sababu makosa ya ugaidi yanahusisha nchi zaidi ya moja.

Kaimu Kamanda wa Kanda hiyo, Daniel Shillah, amesema hayo wakati akizungumza na Nipashe iliyotaka kufahamu mpaka sasa nini kinaendelea dhidi ya kesi hiyo na ni watu wangapi wanaendelea kushikiliwa.

Kuhusu walioshikiliwa mpaka sasa, Kamanda Shillah amesema wanapoona mtu hausiki wanamwachia.

Hata hivyo, Shillah hakutaka kutoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na upelelezi wa tukio nje ya Tanzania.

“Tunashikilia watu watatu au wanne na huenda baadaye tukawaachia wote kulingana na upelelezi unavyokwenda, hatuwezi kuwaachilia mtu mmoja halafu tukaita waandishi wa habari,” alisema.

Tukio la Hamza kushambulia askari na kuua wanne na kujeruhi watu wengine sita lilitokea wiki mbili zilizopita katika eneo la Selander, jijini Dar es Salaam.

Hamza akiwa na silaha awali aliwashambulia askari wawili waliokuwa kwenye kibanda chao maeneo hayo ya Selander kisha akachukua silaha zao mbili aina ya pistol na kuanza kurusha ovyo risasi na kusababisha vifo vingine viwili vya askari na kuwajeruhi watu sita.

Mauaji hayo yalitokea wakati Hamza akirushiana risasi na polisi karibu na Ubalozi wa Ufaransa ambapo polisi walimuua na ndipo baadhi ya ndugu zake akiwamo mama na wadogo zake waliposhikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano na baadhi yao kuachiwa na wengine kuendelea kubaki.

Waliouawa katika tukio hilo ni askari watatu wa Jeshi la Polisi na mmoja kutoka kampuni ya ulinzi binafsi.

Chanzo: ippmedia.com