Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi vigogo Six Telecoms wakamilika

50649 Pic+vigogo

Fri, 5 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili vigogo wa kampuni ya mawasiliano ya Six Telecoms, Limited akiwemo wakili Dk Ringo Tenga, umedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Wakili wa Serikali, Patric Mwita amedai leo Aprili 5, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na ofisi ya mashtaka inaandaa nyaraka ili shauri hilo lianze kusikilizwa.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa, upelelezi umekamilika kinachosubiriwa ni ofisi ya mashtaka kuandaa nyaraka stahiki ili shauri lianze kusikilizwa," amedai Wakili Mwita.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 17 mwaka huu itakapotajwa tena na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalomkabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni mhandisi Hafidh Shamte au Rashid Shamte ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha na kampuni ya Six Telecoms.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita likiwemo la utakatishaji fedha.

Katika kesi ya msingi, Dk Tenga ambaye ni mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni hiyo na wenzake wanadaiwa kuwa, kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa chini ya kiwango cha Dola 0.25 kwa dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao, wanadaiwa katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti Dola 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shitaka la utakatishaji fedha, Hafidh, Noni, Tenga na Chacha, wanadaiwa kuwa walitumia ama walisimamia Dola 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashitaka yaliyotangulia.

Pia, washitakiwa hao wanadaiwa kuwa waliisababishia TCRA hasara ya Dola 3,748,751.22 (sawa na Sh8 bilioni).

 



Chanzo: mwananchi.co.tz