Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya wabunge Chadema, wenzao wakamilika

49413 Jualikalipic

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Upelelezi wa kesi inayowakabili wabunge wawili wa Chadema, Susan Kiwanga (Mlimba), Peter Lijualikali wa Kilombero na wenzao 11 umekamilika ambapo upande wa Jamhuri umekusudia kupeleka mashahidi 12 na vielelezo vinne.

Akisoma maelezo ya awali ya kosa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Elizabert Nyembele leo Ijumaa Machi 29, 2019 wakili wa Serikali Calistus Kapinga amedai katika kesi hiyo ya jinai namba 43 ya mwaka 2019 wabunge hao na wenzao 11 walichoma moto ofisi ya Serikali ya kijiji cha Sofi na kuharibu mali nyingine zenye thamani ya zaidi ya Sh68 milioni.

Wakili Kapinga amedai washtakiwa hao walitenda makosa hayo Novemba 26, 2017, katika kijiji cha Sofi Wilaya ya Malinyi huku wakipinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Sofi.

Kwa upande wake wakili anayewatetea washtakiwa hao Hekima Mwasipu ameomba mahakama kuamrisha upande wa Jamhuri kuleta mashahidi kwa wakati na kama ilivyopangwa ili kuepuka usumbufu na gharama za nauli wanazoingia washtakiwa hao ambao wote wanaishi Malinyi.

“Mhe hakimu wateja wangu wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya nauli na malazi kwa kuwa wanatoka mbali naomba upande wa mashtaka ulete mashahidi kama ilivyopangwa na mahakama, isije ikatokea kama mara ya kwanza mashahidi walikuwa wanasuasua,” amedai Wakili Mwasipu.

Wakili huyo amedai kuwa upande wa mashtaka umekuwa na kawaida ya kuchelewesha mashahidi ama kutowapeleka kabisa kwa wakati jambo ambalo linasababisha hasara kwa wateja wake na pia uchelewaji wa kesi.

Related Content

Naye hakimu Nyembele ameutaka upande wa Jamhuri kuhakikisha wanaleta mashahidi wanne wa kuanzia ambao watasikilizwa Mei 2 na 3, 2019 mahakamani hapo.



Chanzo: mwananchi.co.tz