Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya vigogo wa Nida haujakamilika

27303 NIDA+PIC TanzaniaWeb

Sat, 17 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya Sh1.2 bilioni inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu bado haujakamilika.

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 18, 2016 lakini hadi sasa upelelezi wake bado haujakamilika.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai leo alisema mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kesi hiyo ambayo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa upelelezi wake bado haujakamilika.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Mashauri aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 13 kwa ajili ya kutajwa.

Oktoba 16  Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Kisutu ilipokea hati ya kifo cha  mshtakiwa wa tatu, Benjamin Mwakatumbula na mwenendo wa kesi dhidi yake ukafutwa.

Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo mbali na Maimu ni Meneja Biashara wa (Nida), Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani.

Mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh1.2 bilioni.

Inadaiwa kwenye shtaka la kwanza, Maimu na Mwakatumbula kati ya Januari 15 hadi 19, 2010 katika makao makuu ya Nida wilayani Kinondoni mkoa wa Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kwa nafasi walizokuwa nazo walitumia madaraka vibaya.

Wanadaiwa waliidhinisha malipo kwa Gotham International Limited (GIL) ya dola za Marekani 2,700,00 bila ya kutumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyowekwa na  Benki Kuu ya Tanzania kinyume cha kifungu cha 19.3 cha mkataba kati ya Nida na GIL, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh3,969,000.

Maimu na Mwakatumbula katika shtaka jingine wanadaiwa kati ya Juni 3 na 5, 2013 katika makao makuu hayo walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya dola za Marekani milioni 1.8 bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya GIL kupata faida ya Sh 106,346,000.

Washtakiwa hao wawili wanadaiwa Juni 20, 2014 katika makao makuu hayo, waliidhinisha tena malipo ya dola za Marekani 675,000 kwa GIL bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha, hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh 42,471,000.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kupitisha malipo mengine ya Sh6 milioni kwa GIL bila ya kupiga hesabu kwa kutumia viwango vya kubadilishia fedha hivyo kuifanya kampuni hiyo kupata faida ya Sh14, 661,676.76.

Maimu na Mwakatumbula wanadaiwa kati ya Januari 15, 2010 na Mei 16, 2015 katika makao makuu hayo ya Nida kwa kuidhinisha malipo kwa GIL ya dola za Marekani bila ya kuzingatia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni waliisababishia mamlaka hiyo  kupata hasara ya Sh167,445,676.76.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz