Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upelelezi kesi ya vigogo CCM wakamilika

51120 Pic+ccm+kesi

Mon, 8 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kuomba  rushwa ya Sh5 milioni na kupokea Sh3 milioni inayowakabili vigogo watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam umekamilika.

Vigogo hao ni Jenifer Mushi ambaye ni Katibu wa CCM Tawi la Amana (47), Devotha Batulake Katibu Kata CCM Ilala (43) na Frank Mang'ati ambaye ni Katibu Hamasa CCM Mkoa wa Dar es Salaam (38).

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Sophia Gura  aliyaeleza hayo leo Jumatatu Aprili 8, 2019 mbele ya Hakimu Mfawidhi, Martha Mpaze.

Hata hivyo, Hakimu Mpaze aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 8, mwaka huu ambapo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali (PH).

Katika kesi hiyo ya jinai namba 250 ya mwaka 2019, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa  Machi 21, 2019, walishawishi rushwa ya Sh 5 milioni kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya Daluni East Africa Transport, Daud Kalaghe ili waweze kumpatia kiwanja namba 41 Y kinachomilikiwa na CCM kwa shughuli za biashara.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Machi 22, 2019 katika eneo la Msimbazi Sekondari washtakiwa hao walijipatia rushwa ya Sh3 milioni kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya Daluni East Africa Transport, Daud Kalaghe ili waweze kumpatia kiwanja namba 41 Y kinachomilikiwa na CCM kwa shughuli ya biashara. Kitu ambacho kinahusiana na shughuli za mwajiri wao. Baada ya kusomewa mashtaka hayo Leo kwa mara nyingine washtakiwa wote walikana.

Washtakiwa  hao, wapo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua na vitambulisho ambao kila mmoja alisaini bondi ya Sh5 milioni.

Miongoni mwa mawakili wanaowatetea washtakiwa hao ni  Greygori Ngano, Afred Tukio na Mashaka Charles. Washtakiwa walikamatwa Machi 21 baada ya kuwekewa mtego na Takukuru.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz